MCC KUINYIMA TANZANIA PESA NI PIGO KWA SERIKALI 'CHANGA' YA MAGUFULI

No comments
Tuesday, March 29, 2016 By danielmjema.blogspot.com

Tanzania imehuzunishwa na hatua ya bodi ya shirika la changamoto za milenia (MCC) kusitisha msaada wake wa awamu ya pili wa dola milioni 472.8 ambazo ni sawa na shilingi trilioni moja pesa za Tanzania.



Waziri wa mambo ya nje wa Tanzania Bw Augustine Mahiga ameelezea kushtushwa kwake na hatua hiyo ya bodi ya MCC akisema "imepuuza hatua kubwa tu zilizopigwa kidemokrasia" nchini humo. ''Inasikitisha kuwa demokrasia yetu inatathminiwa tu na matokeo ya uchaguzi wa visiwani Zanzibar,''

Kuhusiana na uchaguzi wa Zanzibar Bw Mahiga anasema kuwa Tanzania, ilifanya kila kitu kuambatana na sheria na katiba ya nchi wala hakuna tatizo ama ukiukwaji wa sheria.
Mahiga anasema kuwa huo ni uamuzi wao na kwa sababu hela hizo ni zao wanauhuru wa kuzitumia watakavyo ila anahoji kwanini uamuzi huo uliafikia bila ya majadiliano na serikali ya muungano ya Tanzania.

Kuhususiana na kupitishwa kwa sheria ya uhalifu wa mitandao bwana Mahiga anasema sheria hiyo ilikuwa inalenga kupambana dhidi ya ugaidi. Waziri huyo ameonya kuwa watu wanaoishi vijijini ndio watakaoathirika zaidi kwani fedha hizo zilikuwa zimepangiwa kueneza umeme mashinani.

Katika kutoa uamuzi wake, Bodi ya Shirika la Changamoto za Milenia (MCC) ilisema kuwa Tanzania haijatimiza viwango vinavyohitajika ili kunufaika na ufadhili kutoka kwa shirika hilo, na hivyo basi haitapokea msaada wa awamu ya pili.

Kupitia taarifa, bodi hiyo ilisema kuwa: "Serikali ya Tanzania haijachukua hatua za kuhakikisha kuheshimiwa kwa uhuru wa kujieleza na uhuru wa kujumuika katika utekelezwaji wa sheria ya Uhalifu wa Mtandao.”

Bodi hiyo aidha imesema Tanzania iliendelea na uchaguzi wa marudio Zanzibar ambao "haukushirikisha wote na wala haukuakisi maoni ya wote, licha ya malalamiko kutoka kwa serikali ya Marekani na jamii ya kimataifa.”

HUWEZI KUWA DIKTETA KABLA HUJAJITEGEMEA KIUCHUMI! (YA TANZANIA NA MISAADA
YA MCC)!

Serikali ya Marekani imesitisha na kuvunja mahusiano yake na serikali ya Tanzania katika mambo yote yanayohusu miradi ya MCC. Katika tamko lilitolewa na bodi ya MCC jana Jumatatu, serikali ya Marekani
imeeleza kusikitishwa kwake na hatua ya Tanzania kutochukua hatua katika masuala mawili muhimu;

1. Kutoendelea kutangaza matokeo halisi ya uchaguzi wa tarehe 25 Oktoba 2015 na hatimaye kumtangaza mshindi na badala yake kuendelea na uchaguzi wa upande mmoja uliofanyika 20 Machi 2016 (tafsiri yangu)

2. Kutositisha matumizi ya sheria ya Makosa ya Mtandao (Cybercrime Act) AU kutoifanyia marekebisho ili iendane na ulinzi wa haki za raia na uhuru wao wa mawasiliano, Marekani imebaini kuwa Tanzania imeendelea kuitumia sheria hiyo mbaya kukandamiza uhuru wa wananchi kimakusudi (tafsiri yangu).

Marekani imesisitiza kuwa moja ya vigezo vikuu vya kupata fedha za MCC ni nchi mshirika kuwa na rekodi ya kuendesha mambo yake kidemokrasia na hasa kufanya chaguzi zilizo huru na haki, jambo ambalo Tanzania imeshindwa.

NINI MAANA YA UAMUZI HUO;

1. Tanzania itakosa Shilingi Trilioni 1 (bilioni 1000) ambazo zilipangwa kuelekezwa kwenye miradi ya umeme na umeme vijijini.

2. Itaipasa serikali kutafute fedha katika maeneo mengine na kuziba shimo lililoachwa na MCC.

3. Kuhalalisha Marekani kuanza kuchukua hatua zingine za kiuchumi dhidi ya Tanzania (ikiwa itaamua kufanya hivyo),

4. Kuzivutia nchi nyingine wahisani kama Umoja wa Ulaya, kutoa misimamo yao na hata kuinyima Tanzania fedha muhimu za kiushirikiano.

HATARI YA KUWA NA BAJETI HOI;

Inafahamika (kwa takwimu za serikali) kwamba hadi mwaka wa fedha uliopita,
bajeti ya Tanzania ilitegemea wahisani kwa zaidi ya asilimia 30. Lakini ukiongea na wachumi na watafiti wa kiuchumi watakueleza kuwa bajeti ya Tanzania ni tegemezi kwa takribani asilimia 50 na zaidi na kwamba tawkimu hizo za serikali ni za kupikwa.

Ndiyo maana kwa miaka takribani 8 mfululizo (kwenye utawala wa JK), sehemu kubwa ya bajeti zilizofikishwa bungeni na serikali kila mwaka hazikutekeleza kwa takribani asilimia 30 hadi 50 (Yaani fedha hizo zilikosekana na kwa hivyo wizara au vitengo husika havikusimamia miradi iliyokuwa inapangwa).

Huo ni ushahidi kuwa nchi yetu inaweza kutangaza kirahisi sana kuwa inajitegemea kiuchumi kwa asilimia  80 lakini ukweli halisi ukawa inajitegemea nusu ya hapo (Kumbuka, ni kawaida sana kwa serikali za
Kiafrika kupika takwimu na kuwafurahisha wananchi wake).

MAREKANI INAINGILIA MAMBO YA NDANI YA TANZANIA?

Kwa wanaojua, katika muktadha wa kimataifa kila taifa linachukuliwa kuwa "Sovereign", yaani lililo huru na lisiloingiliwa hasa kwa mambo yake ndani.

Nadhani kwa hatua hizo, Marekani haingilii uhuru wa Tanzania bali inaifanya Tanzania ikumbuke kuwa moja ya masharti ya kupata misaada yao ni kusimamia demokrasia kwa mapana yake, Tunakumbushwa.

Na hii ni ishara ya amri kuwa kama tunataka kuendesha mataifa yetu kidikteta na kutupa haki za kiraia baharini, tunao wajibu wa kujenga uchumi imara usio tegemezi ili "tuwe madikteta wa kudumu".

Marekani inatupatia somo kuwa kama tunaamini dunia ni kijiji chetu peke yetu, na tuendelee kuishi humo kijijini.

KUHUSU MISAADA!

Inafahamika, kwamba wengi wetu na hata mimi tunaamini katika kujitegemea kiuchumi kuliko kuendelea kupigia magoti misaada ya wahisani. Lakini inafahamika pia kwamba wengi wetu hatukubaliani kabisa na "uhuni na uporaji wa demokrasia uliofanywa Zanzibar ukisimamiwa na serikali ya Zanzibar na hii ya Muungano" na kwa hivyo si ajabu wengi wetu kwa muktadha huo tukaunga mkono hatua za mataifa ya Magharibi juu ya kataifa haka ambako bado ni ombaomba na bado hakatimizi hata masharti ya kuendelea kuomba kwa wakubwa.

Habari Zingine

0 MAOINI :

Fadhili Athumani



EastAfrica Swahili Blogger, Journalist at Mwanaspoti Kenya, Nairobi Kenya, Call: +254705246475, whatsapp:+255654724337, Email: fadhiliathumani85@gmail.com

Proudly Powered by EAMG .