KIFO CHA SAITOTI, ILIKUWA NI AJALI YA KAWAIDA AU ALIUWAWA?
Posted in
afrika mashariki
No comments
Thursday, April 14, 2016
By
danielmjema.blogspot.com
KATIKA makala ya leo, tunaangalia, kifo cha jabari la siasa za Kenya na Makamu wa Rais aliyehudumu kwa muda mrefu (miaka 13) chini ya uongozi wa Rais wa pili wa Kenya, Daniel Toroitich Arap Moi ambaye pia kbala ya kifo chake alikuwa ni Waziri wa Usalama wa ndani, Prof. George Saitoti (66). Je, Saitoti alikufa kifo cha kawaida au aliuwawa? je nani aliyemuua Saitoti?
Hili ni swali ambalo bado limetawala vichwa vya wakenya wengi, huku zikiwa zimetimia takribani miaka minne tangu Ajali ya Helikopta iliyopelekea kifo cha Saitoti na Mwanasiasa mwengine nguli, Orwa Ojode. Ilikuwa ni Juni 10, mwaka 2012 ambapo Vilio na majonzi nchini Kenya vilihanikiza.
Katika ajali hii iliyokatisha maisha na ndoto za Prof. Saitoti, watu wengine watano waliokuwepo kwenye helikopta hiyo nao walifariki akiwepo Naibu wake Orwa Ojode, walinzi na marubani.Saitoti na naibu wake Orwa walikuwa wakielekea katika mkutano wa kiusalama katika eneo la Sotik magharibi mwa Kenya.
Mengi yamesemwa lakini ukweli kuhusu kifo cha Saitoti ambaye alikuwa ni mmoja wa wanasiasa wenye nguvu nchini Kenya huku akidaiwa kuwa miongoni mwa watu waliotangaza nia ya kuwania kiti cha Urais, kwenye Uchaguzi mkuu wa mwaka 2013, bado haujajulikana japo kuna madai kwamba eti, Saitoti aliuwawa.
Licha ya Serikali kuanisha tume ya kuchunguza kiini cha ajali ya Helikopta hiyo iliyoondoka na uhai wa Prof. Saitoti na Naibu wake Ojode, dhana kwamba Ajali hiyo ilikuwa ni mpango uliopikwa kwa lengo la kumuondoa Prof. Saitoti ambaye wakati huo alikuwa tishio kwa baadhi ya 'mapapa' wa siasa haiepukiki.
Katika Bunge la Kenya, Wabunge waliituhumu wazi wazi Serikali ya Rais Mwai Kibaki kwa kile walichodai kuwa ilikuwa ikiikwaza wazo la mauaji ya kupangwa (planned Assassination) kwa kuinyima uhuru tume iliyokuwa ikichunguza kifo cha mwanasiasa huyo jambo linalozidi kuzua maswali kama vile, je Saitoti alikuwa ni tishio kwa Serikali ya Mwai Kibaki? Je, uchaguzi wa mwaka 2013 ungekuwa na matokeo ya tofauti endapo Saitoti angekuwa hai?
Kumekuwa na madai kwamba, Familia ya Wabunge hao waliofariki (Saitoti na Ojode), wamekuwa wakizuia kufuatilia namna ambavyo uchunguzi wa vifo vya ndugu zao inavyoendelea ambapo hata mara moja inadaiwa hawajahusishwa.
Taarifa nyingine zinasema kuwa hata wataalamu wa milipuko na wataalamu wa Helikopta, Chris Briers na Tim Carter, ambao waliletwa na familia ya Saitoti kuungana na timu ya serikali iliyokuwa ikichunguza vifo hivyo, ilibidi warudi zao makwao, Afrika Kusini kwa kukosa ushirikiano.
Wakati uchunguzi huo ukiendelea, familia ya Saitoti iliomba mabaki ya Helikopta hiyo yahifadhiwe kwenye sanduku maalum (4 foot container) hadi hapo itakapofanyiwa uchunguzi wa kina, lakini ikadaiwa kuwa zoezi hili lilishindikana kutokana na Serikali ya Rais Kibaki, ilishindwa kutoa fedha zilizohitajika kununulia Sanduki hiyo (Ksh 70,000).
Katika kufuatilia swala hilo, wakili wa familia ya Saitoti, Bw. Fred Ngatia, aliingilia kati kuzuia mitambo ya Helikopta hiyo kusafirishwa hadi nchini Ufaransa kwa ukaguzi na uchunguzi lakini juhudi zake hazikuzaa matunda kwani hakukuwa na mawasiliano chanya kati yake na Serikali.
Aidha, kulikuwa na madai na shutuma kutoka kwa Wabunge kuwa hata timu ya wataalamu kutoka Ufaransa waliokuja nchini kufuatilia kiini cha ajali hiyo, walikwazwa na kunyimwa ushirikiano na serikali kiasi cha kuamua kurudi zao na kuachana na zoezi la kufuatilia kifo cha Prof. Saitoti.
Mengi yamesemwa, lakini miaka minne tangu ajali hii ambayo imeacha majonzi katika mioyo ya wakenya na maswali mengi yasiyokuwa na majibu. Swali la kutuongoza hapa ni Je, kuna ushahidi wowote ambao unaweza kutuaminisha kuwa kifo cha Saitoti kilipangwa kumzima kisiasa (Political assassination) hasa ukizingatia Prof. Saitoti, alikuwa ni mgombea mtarajiwa kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2013?
Muda mfupi kabla ya ajali hiyo, iliyotokea katika msitu wa Ngong, kuna ushahidi kuwa mlinzi wa Saitoti (Bodyguard), ambaye alikuwa kwenye na Saitoti kwenye Helikopta alimpigia simu Dereva wa Waziri huyo wa Usalama wa ndani, akimtaka kuwasubiri katika uwanja wa ndege wa Wilson kwani Helikopta hiyo ambayo ilitokea uwanjani Wilson, ilikuwa na matatizo na hivyo ilikuwa njiani kurudi Wilson.
Hii inamaana gani, maana yake ni kwamba abiria wote katika Helikopta hiyo, walikuwa na taarifa mapema kwamba ndege yao ilikuwa na matatizo ya kimitambo hivyo inawezekana kabla ya ajali walikuwa wameshaamua kuahirisha safari yao.
Tuchukulie kwa mfano kwamba hali ilikuwa hivyo, wapelelezi na timu ya uchunguzi wa chanzo cha ajali hiyo, wanaweza wakahitimisha kuwa, ilitokana na hitilafu ya mitambo ambayo ilimlazimu Rubani kuamua kurudisha Helikopta Nairobi, dakika 10 tu baada ya kuanza safari.
Kitu ambacho kinazidi kuzua utata ni kwamba, siku chache kabla safari ya Saitoti na Naibu wake, Rubani Helikopta hiyo, Bi. Gituanja, aliijaribisha Helikopta hiyo ambapo Juni 7, mwaka 2012, aliruka nayo, kutoka Wilson hadi Voi na kurudi salama na kuridhika ndege yake iko katika hali nzuri.
Hivyo basi, kama Helikopta hiyo iliweza kuruka salama masaa 72 kabla ya kuungua na kusababisha vifo vya Saitoti na wenzake, je nini kilitokea muda mfupi baada ya rubani kujaribisha ndege na kuirudisha Wilson? Inadaiwa kuwa siku ya tukio, wakati Chopa hiyo inaanza safari, ikiwa ndani ya dakika 2-3 baada ya kuanza kuruka uwanjani Wilson, iliyumba.
Hii inamaanisha kwamba, kulikuwa na tatizo kabla ya kuanza kuruka kwa sababu ilikuwaje Chopa iyumbe kabla ya kuondoka, Helikopta iliweza kuruka lakini muda mchache ikiwa hewani ghafla rubani aliamua kusitisha safari.
Kutokana na hali halisi, swali ambalo wachunguzi watahitaji kuhoji ni kipi hasa kilisababisha Chopa iyumbe? kwa sababu inawezekana tatizo hilo ndilo lililopelekea Chopa kuanguka na kulipuka na pia ndio sababu hata Rubani alitaka kuahirisha safari.
Hali halisi ni kwamba: “Safari ilianza pale Wilson Airport, Nairobi majira ya saa 2:32 asubuhi, katika hali ya hewa nzito, yenye kuruhusu kuona umbali wa kilomita 8, Rubani alipoteza mawasiliano na kitendo cha mawasiliano ya ndege, majira ya saa 2:38 asubuhi, na dakika nne baadaye, ndege ilianguka," Waziri wa Uchukuzi (wakati huo), Amos Kimunya aliliambia baraza la mawaziri, kupitia runinga ya KTN.
Swali ambalo maafisa usalama waliokuwa wanachunguza tukio hili ni aina ya hitilafu ya kiufundi iliyosababisha ndege ya aina hiyo, kupata ajali dakika sita baada ya kuruka. Aidha dhana ya kuwepo kwa hitilafu ya kiufundi, imepuuzwa vikali na kampuni iliyoitengeza, wakisema kuwa Chopa hiyo ilikuwa na uwezo wa kutua salama hata baada ya kuyumba au baad aya kutokea kwa hitilafu yoyote ya kiufundi (ability to glide and land).
Katika kuthibitisha madai yao kwa maafisa wa Kenya, wataalamu waliobuni ndege hiyo, walirusha ndege nyingine inayofanana na Chopa iliyopata ajali, umbali wa 3,500ft, wakazima Injini yake, na ikaweza kutua salama bila tatizo lolote.
HISTORIA YA SAITOTI
Saitoti, katika medani za kisiasa nchini Kenya, alitumia nafasi ya elimu yake katika kumpandisha katika ulingo wa kisiasa na hatimaye mwaka 1983 alichaguliwa kuwa mbunge nchini humo chini ya uongozi wa aliyekuwa rais wa Kenya, Daniel Arap Moi. Baada ya miaka mitano Saitoti alichaguliwa kuwa makamu wa rais.
Taarifa nyingine zinasema kuwa Saitoti alitokea kupata umaarufu kutokana na utendaji wake wa kazi, unyenyekevu na uaminifu kwa rais Moi, jambo ambalo lilimshawishi Moi kuendelea kumweka madarakani kwa miaka 13.
Mwanzoni mwa miaka ya 1990, wakati bado akiwa makamu wa rais na waziri wa fedha, Saitoti alihusishwa na kashfa ya rushwa iliyojulikana kama “Goldenberg Scandal” – udanganyifu uliofanywa katika serikali kiasi cha kuathiri uchumi wa Kenya kupungua kwa asilimia kumi katika mapato yake ya mwaka.
Hiyo ilikuwa kashfa iliyomchafua sana Saitoti kwa kipindi chote alichokuwa madarakani japokuwa kuhusika kwake katika kashfa hiyo hakukuweza kuthibitishwa moja kwa moja.
Saitoti alijiuzulu kuwa waziri wa elimu Februari 2006, lakini akachaguliwa tena kushika nafasi hiyo mwezi mmoja baada ya mahakama ya sheria nchini humo kuamua kuitupili mbali kashfa iliyokuwa ikimkabili ya kuhusihwa katika rushwa.
Baada ya maamuzi hayo ya mahakama, Saitoti alisema kuwa alihisi kuwa huru na kutua mzigo mkubwa, ambao alikuwa ameubeba kwa zaidi ya muongo mmoja. Hata hivyo, serikali ilisema itakata rufaa dhidi ya hukumu hiyo, lakini haikufanya hivyo.
Pamoja na kashfa hiyo kutikisa, Saitoti hakukata tamaa na hatimaye akateuliwa kuwa mmoja wa “makamanda” walioaminika katika serikali ya rais wa sasa wa Kenya, Mwai Kibaki. Akiwa ndani ya serikali ya Kibaki, Saitoti alichaguliwa kuwa waziri wa elimu na hatimaye kuwa waziri wa usalama wa ndani wa Kenya, ambapo alikuwa msemaji mkuu wa serikali katika masuala ya usalama wa nchi hiyo.
Saitoti alichaguliwa na serikali yake katika kuongoza mapambano dhidi ya kikundi cha kigaidi cha Somalia cha al-Shabab, ambacho kinaaminika kuhusika katika mashambulizi mbalimbali yanayotokea ndani ya Kenya.
Saitoti alionekana mara kwa mara katika televisheni ya taifa akielezea uamuzi wa nchi yake katika kupambana na kikundi cha al-Shabab. Wachambuzi wa masuala ya siasa wanasema kuwa alitimiza wajibu wake katika kufanya maamuzi hayo.
Katika kile kinachoonekana kukubalika katika ulingo wa siasa nchini Kenya, utendaji kazi wa Saitoti ulimweka katika nafasi ya kugombea kiti cha urais wa nchi hiyo katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mwakani.
Wachambuzi wa masuala ya siasa wanasema kuwa kifo chake kinaweza kusababisha matatizo ndani ya serikali ya nchi hiyo. Ikumbukwe pia kuwa serikali ya Kenya ilikumbwa na machafuko ya kisiasa katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2007.
Ni serikali ambayo haijawa na urahisi na kutulia katika siasa za uadui ambayo kwa sasa inasemekana kuwa baadhi ya wanasiasa wamekuwa wakitafuta kura za kikabila wakati wa kuelekea uchaguzi mkuu mwakani.
Lakini si kwa Saitoti; akiwa na asili ya mchanganyiko wa damu ya Masai na Kikuyu, inasemekana hakuwa na kundi lolote la kikabila, na wala hakuwahi kujaribu kufanya hivyo, badala yake alifanya kazi ya kuunda kundi la wanachama walio na nguvu.
Siasa za Kenya sasa zimeingia katika mapungufu, na inaonekana kwamba haitakuwa rahisi kupata mtu mwingine wa kuziba nafasi iliyoachwa na Saitoti, na kuimarisha makundi aliyoyaita kuwa ni yake.
Taarifa nyingine toka nchini humo zinasema kuwa, ingawa bado muda wa kampeni haujafika rasmi, baadhi ya wanasiasa wameanza kupiga kampeni, jambo ambalo linaonekana litasababisha uchaguzi huo kuwa moja kati ya chaguzi za hatari na zenye vurugu ambazo Kenya haijawahi kushuhudia katika historia yake.
Wakati hayo yakitokea, serikali imetangaza siku tatu za maombolezo kutokana na msiba huo.
“Kifo cha Saitoti ni pigo kubwa sana na kimeiangusha serikali yetu katika kipindi hiki ambacho tupo katika maandalizi ya kufanya uchaguzi mkuu wa amani,” alisema Waziri Mkuu wa Kenya Raila Odinga katika eneo la ajali Kibiku takriban kilomita 20 kutoka mji mkuu wa Nairobi.
Bado haijulikana chanzo cha ajali hiyo cha helikopta hiyo kuanguka. Polisi wapo katika uchunguzi wa ajali hiyo. “Mpaka tunapoongea sasa, hakuna mtu anayejua chanzo cha ajali hii na uchunguzi bado unaendelea,” alisema Odinga. Alisema kuwa Saitoti na naibu wake Orwa walikuwa wakielekea katika mkutano wa kiusalama katika eneo la Sotik magharibi mwa Kenya.
Naye Johnnie Carson, Katibu msaidizi wa Marekani katika masuala ya Afrika, wakati alipoitembelea Kenya Jumapili iliyopita alisema kuwa nchi hiyo imempoteza mtumishi aliyekuwa na msisimamo na mpiginaji mkuu na kwamba nchi yake imetuma salamu za rambirambi nchini Kenya.
Aidha, kiongozi ambaye anajulikana kuwa ni mpinga rushwa nchini Kenya, Mwalimu Mati alisema kuwa tukio hilo liifanye nchi hiyo kutilia mkazo katika kupinga historia ya serikali ya kipuuzi ambayo imekuwa ikinunua helikopita za kipolisi.
Alisema kuwa helikopta hizo zina gharama kubwa na pia gharama za matengezo zimekuwa kubwa na kuongeza kuwa vitu hivyo vimegharamu nchi hiyo mamilioni ya dola tangu mwaka 1999.
Habari Zingine
Mjulishe Mwenzako
0 MAOINI :