MCHAKATO WA KUMPATA MRITHI WA BAN KI-MOON WAANZA
Posted in
Siasa
No comments
Wednesday, April 13, 2016
By
danielmjema.blogspot.com
Kwa mara ya kwanza Umoja wa Mataifa umeweka wazi mchakato wa kuwania
nafasi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa baada ya kutoa nafasi kwa
mataifa yote kuwauliza maswali wagombea waliojitokeza kuwania nafasi
hiyo.
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa |
Wagombea watatu miongoni mwa tisa waliojitokeza kuwania nafasi hiyo walipata nafasi ya kuulizwa maswali na kuelezea mipango yao ya baadaye katika utendaji wao iwapo watafanikiwa kushika nafasi hiyo baada ya kumalizika muda wa uongozi wa Katibu Mkuu wa sasa Ban Ki-moon hapo January 1, mwakani.
Kwa miongo kadhaa sasa mchakato wa uchaguzi wa nafasi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa umekuwa ukifanyika katika mazingira ya siri chini ya usimamizi wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linaloundwa na wajumbe kutoka nchi wanachama wa baraza hilo ambazo ni pamoja na Uingereza, Ufaransa, China, Urusi na Marekani.
Katibu Mkuu wa sasa wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon |
Hata hivyo, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka jana lilipiga
kura kubadilisha utaratibu huo na kuwataka wagombea wa nafasi hiyo
kuwasilisha barua za maombi, kutoa muhtasari wa malengo yao pamoja na
kuwa tayari kujieleza na kuulizwa maswali.
Uamuzi wa mwisho wa uteuzi wa nafasi hiyo bado unabakia katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, lakini hatua hiyo ya kuweka uwazi katika mchakato huo utaweka msukumo kwa mataifa hayo yenye nguvu kuteua jina la mtu ambaye atakuwa anakubalika kwa kiwango kikubwa.
Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Mogens Lykketoft alisikika akisema kuwa haya ni mabadiliko muhimu. " Iwapo kutakuwa na idadi kubwa ya nchi zinazomuunga mkono mgombea mmoja sidhani kama Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litakuja na jina tofauti na hilo " alisema.
Waziri wa Mambo ya nje wa Montenegro Igor Luksic mwenye umri wa miaka 39 ambaye ni mgombea kijana kuliko wote waliojitokeza kuwania nafasi hiyo alikuwa wa kwanza kujieleza mbele ya wajumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa akielezea jinsi atakavyotumia uzoefu wake wa nafasi alizowahi kushika katika nchi yake ikiwemo uwaziri mkuu katika kuwania nafasi hiyo.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la sayansi, Elimu na Utamaduni-UNESCO Irina Bokova pamoja na mtendaji mkuu wazamani wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshugulikia masuala ya wakimbizi ambaye pia amewahi kuwa Waziri Mkuu wa Ureno Antonio Guterres ni miongoni mwa waliopata nafasi ya kujieleza mbele ya baraza hilo.
Habari Zingine
Mjulishe Mwenzako
0 MAOINI :