CORD sasa kuandamana siku ya Madaraka Day

No comments
Monday, May 23, 2016 By danielmjema.blogspot.com

BAADA ya kulitikisa taifa na Maandamano makubwa ya kushinikiza maafisa wa IEBC kung'atuka, yaliyofanyika katika Jiji la Nairobi na miji ya Kisumu, Mombasa, Kakamega na Siasa, Muungano wa Upinzani (CORD) sasa umepanga kufanya maandamano mengine makubwa siku ya maadhimisho ya Madaraka Day.
Akizungumza na waandishi wa habari nje ya Ofisi za CORD, zilizoko Capital Hill, mara baada ya kumalizika kwa maandamano ya leo (Jumatatu, Mei 22, 2016), Kiongozi wa CORD, Raila Odinga alisema kuwa kamwe hawatatishika na matumizi makubwa ya nguvu yanayofanywa na Jeshi la Polisi kwa lengo la kuwazuia kuzifikia Ofisi za IEBC, zilizoko Anniversary Towers na kwenye makaunti.
“Tangazo lililotolewa na Polisi kuwa hawakujulishwa mapema kuhusu maandamano yetu ni maelezo ya kipumbavu ambayo yamepelekwa vifo vya raia wema, Muungano wa Jubilee walienda mahakamani kutafuta kibali cha kutuwekea zuio, lakini kwa bahati nzuri haki ilikuja upande wetu, hili linatupa kiburi kwamba maandamano yetu yalikuwa ni ya haki na yalizingatia sheria," alisema Raila.
Waziri mkuu huyo wa zamani, alisema kuwa kitendo cha Serikali hapo nyuma kushindwa kuwafungulia mashitaka Polisi waliohusika katika kuwafyatulia risasi wananchi wakati wa vurugu vya baada ya uchaguzi, mwaka 2007/2008, ndivyo vinavyopelekea Polisi kuchukulia mazoea ya kuwaonea wananchi wakijua mwisho wa siku hakuna mtu wa kuwawajibisha.
Wakati huo huo, Mwanamume mmoja amefariki wakati wa maandamano ya upinzani katika mji wa Kisumu, magharibi mwa Kenya. Mwanamume huyo anadaiwa kufariki wakati wa makabiliano kati ya polisi na waandamanaji hao wanaowashinikiza maafisa wa Tume ya Uchaguzi (IEBC) kujiuzulu.
Hospitali moja mjini humo imethibitisha kwamba mwili wa mwanamume umefikishwa katika hospitali hiyo lakini chanzo cha kifo chake hakijathibitishwa. Jijini Nairobi, maafisa wa polisi wametawanya waandamanaji waliokuwa wakitaka kufika katika afisi kuu za tume hiyo.

Shughuli za kibiashara katika jiji hilo zimetatizika pakubwa.Polisi wamekuwa wakikabiliana na makundi ya wafuasi wa muungano huo wa upinzani wa Cord kwa mabomu ya kutoa machozi na maji ya kuwasha. Maandamano pia yameshuhudiwa katika miji mingine kama vile Mombasa na Kakamega.
Viongozi wa CORD wanasema mmoja wa maseneta wa muungano huo amekamatwa wakati wa maandamano ya leo mjini Kakamega, magharibi mwa Kenya. Leo imekuwa wiki ya nne ya maandamano hayo ya upinzani.Wiki iliyopita, polisi walikabili vikali waandamanaji na baadaye walishutumiwa na mashirika ya kutetea haki za kibinadamu kwa kutumia "nguvu kupita kiasi”.
Rais Uhuru Kenyatta wiki jana alisema upinzani unafaa kutumia utaratibu uliowekwa kikatiba iwapo unataka kufanikisha mabadiliko katika tume ya uchaguzi. Ametoa wito kwa “upinzani kuonesha siasa komavu badala ya kutumia njia haramu kuvutia hisia.”

Habari Zingine

0 MAOINI :

Fadhili Athumani



EastAfrica Swahili Blogger, Journalist at Mwanaspoti Kenya, Nairobi Kenya, Call: +254705246475, whatsapp:+255654724337, Email: fadhiliathumani85@gmail.com

Proudly Powered by EAMG .