Mataifa yakutana kuijadili IS nchini Libya
Posted in
Kimataifa
No comments
Monday, May 16, 2016
By
danielmjema.blogspot.com
Mataifa kadhaa yenye nguvu duniani yanakutana leo katika mji mkuu wa Austria, Vienna kujadili kuongezeka kwa ushawishi wa kundi linalojiita Dola la Kiislamu, IS nchini Libya, ambako ni kitisho kwa Ulaya.
Mkutano huo unaongozwa kwa pamoja na Marekani pamoja na Italia ambayo ni mkoloni wa zamani wa Libya, na ambayo imekuwa ikitaabika kutokana na idadi kubwa ya wahamiaji wanaoingia kwenye ardhi yake, wakitokea Afrika Kaskazini.
Msemaji wa wizara ya mambo ya nchi za nje ya Marekani John Kirby, amesema mkutano huo wa leo utatakafari msaada ya jumuiya ya kimataifa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya, kwa kuangazia zaidi masuala ya kiusalama.
Wenyekiti wa mkutano huo ni waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry, na mwenzake wa Italia Paolo Gentiloni. Gentiloni amesema kabla ya mkutano huo, kuwa nguvu za pamoja zinahitajika kusaidia mchakato wa kurejesha utulivu nchini Libya.
Uungwaji mkono nje, upinzani ndani
Serikali hiyo inayoongozwa na mfanyabiashara Fayez al-Sarraj inaungwa mkono kimataifa katika juhudi za kuiunganisha tena nchi, lakini inakabiliwa na upinzani wa ndani.
Bado haiungwi mkono na bunge lililochaguliwa nchini humo, na mtu aliyetangaza kuwa mkuu wa majeshi Khalifa Haftar, mshirika wa bunge hilo ambaye ameapa kuyaangamiza makundi ya kiislamu nchini Libya.
Hata serikali kinzani yenye makao mjini Tripoli imekataa kuitambua serikali hiyo ya umoja wa kitaifa.
Katika mazingira hayo ya mgawanyiko, IS imejiimarisha katika eneo linalouzunguka mji wa Sirte kwenye ufukwe wa Mediterania, ambao imeugeuza kituo cha mafunzo kwa wanajihadi kutoka maeneo yote ya karibu na ya mbali.
Tumbo joto kwa Ulaya na Marekani
Ulaya ina wasiwasi kwamba wanajihadi hao ambao wamekuwa wakijikusanya upya, watautumia uwanja wa ndege wa Sirte na bandari ya mji huo, kuanzisha mashambulizi dhidi ya bara la Ulaya.
Hivi karibuni ripoti ya bunge la Uingereza ilisema kuwa operesheni ya Umoja wa Ulaya baharini kupambana na magenge yanayosafirisha watu kimagendo imeshindwa.
Wasiwasi huo unakwenda sambamba na hofu ya Marekani, ambako maafisa wa serikali na wanadiplomasia wamesema ipo mipango ya kufikiria jinsi ya kuiondolea Libya vikwazo vya kuagiza silaha kutoka nje, ambavyo iliwekewa na Umoja wa Mataifa miaka mitano iliyopita.
Afisa mmoja wa ngazi ya juu wa Marekani ameliambia shirika la habari la AFP, kwamba washirika wako tayari kuisaidia serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya, ikiwa itatoa maelezo ya kutosha na yenye kueleweka, juu ya namna inavyopanga kupambana na kundi la Dola la Kiislamu.
Maelezo hayo ndio yanayotarajiwa kuzungumziwa na Kerry na wenzake katika mkutano wa Vienna, lakini kuna mashaka ikiwa serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya itawasilisha mpango kamili wa kutaka usaidizi.
Nguvu zilizotawanywa
Mgawanyiko nchini Libya ulizidi makali hivi karibuni, pale pande mbili zinazopingana, serikali ya Umoja wa Kitaifa, na vikosi vinavyoongozwa na Khalifa Haftar, zilipotangaza mipango ya kupambana na IS, kila upande kivyake.
Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi katika baraza la seneti la Italia Nicola Latorre alisema hali hiyo ni kosa linalopaswa kuzuiliwa, na kuongeza kuwa hawataendelea kuukubali mgawanyiko huo.
Suala jingine litakalojadiliwa katika mkutano wa Vienna ni la wahamiaji haramu wanaoendelea kumiminika Ulaya, na mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini amesema atajadili uwezekano wa kurefusha operesheni ya kupambana wa wasafirishaji haramu wa watu hao.
Mwandishi: Daniel Gakuba/afpe
Source: DW Kiswahili
Habari Zingine
Mjulishe Mwenzako
0 MAOINI :