Wasiwasi DR Congo muhula wa Kabila ukifikia kikomo

Posted in
No comments
Monday, December 19, 2016 By danielmjema.blogspot.com

Mzozo wa kisiasa unaendelea kutokota nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo huku muhula wa Rais Joseph Kabila ukifikia kikomo leo, kwa mujibu wa katiba. Mazungumzo ya kutafuta suluhu kati ya serikali na upinzani yaliahirishwa wiki iliyopita baada ya kukosekana kwa mwafaka. 
Mazungumzo hayo yanayoongozwa na maaskofu wa kanisa Katoliki yanatarajiwa kurejelewa Desemba 21. Kuna wasiwasi kwamba huenda kukatokea maandamano Jumatatu wafuasi wa upinzani wakipinga kuendelea kusalia madarakani kwa Bw Kabila.
Upinzani unamlaumu Rais Kabila ukisema ndiye aliyechangia mzozo wa sasa kwa kujaribu kukwamilia madaraka. Watu zaidi ya 50 waliuawa kwenye maandamano ya upinzani mwezi Septemba. Maafisa 3 wa polisi pia waliuawa kwenye maandamano hayo.
Rais Kabila amesema ataendelea kusalia madarakani kwani uchaguzi mkuu haukufanyika ilivyotarajiwa mwezi Novemba na hivyo basi hakuna mrithi aliyechaguliwa.
Wanajeshi na maafisa wa polisi wameweka vizuizi kwenye mji mkuu Kinshasa, kukiwa na wasiwasi wa kutokea tena kwa maandamano na ghasia.Serikali iliagiza kampuni za mawasiliano kufungia mitandao ya kijamii na imeahidi kukabiliana vikali na waandamanaji.
Waziri wa mawasiliano Lambert Mende ameambia BBC: "Kabila atasalia madarakani hadi rais mpya achaguliwe. Hakuna jambo jingine litakalofanyika. Mtu akijaribu kuvuruga amani hapa mjini, atakumbana na polisi kama inavyofanyika maeneo mengine duniani."
Uchaguzi uliahirishwa hadi 2018, hatua ambayo upinzani unasema ni jaribio la Bw Kabila la kutaka kusalia madarakani. Kwa mujibu wa katiba, muhula wa pili wa Rais Kabila, aliyeingia madarakani baada ya kuuawa kwa babake Laurent Kabila mwaka 2001, unafaa kumalizika tarehe 19 na kuwe na rais mpya 20 Desemba. 
Mwaka uliopita, watu 12 waliuawa katika maandamano ya upinzani. Tangu kujinyakulia uhuru zaidi ya miaka 55, hakuna kiongozi aliyewahi kumkabidhi mrithi wake madaraka kwa njia ya amani.

BBC

Habari Zingine

0 MAOINI :

Fadhili Athumani



EastAfrica Swahili Blogger, Journalist at Mwanaspoti Kenya, Nairobi Kenya, Call: +254705246475, whatsapp:+255654724337, Email: fadhiliathumani85@gmail.com

Proudly Powered by EAMG .