WATU WATATU WAKAMATWA TUHUMA ZA KUSAFIRISHA WATOTO 10 MKOANI KILIMANJARO
Posted in
No comments
Wednesday, June 6, 2012
By
danielmjema.blogspot.com
JESHI la polisi Mkoani Kilimanjaro linawashikilia watu watatu
(3), kwa tuhuma za kusafirisha na kuwatumikisha watoto wenye umri chini ya
miaka 15, kwa ajili ya kulima na kupalilia matuta ya vitunguu wilayani Same, Mkoani
Kilimanjaro.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa kwa vyombo vya habari, kamanda
wa polisi mkoani Kilimanjaro, Robert Boaz, alisema jeshi hilo lilipata taarifa
kutoka kwa raia mwema, kwamba kuna watoto 10 waliochini ya miaka 15 wamehifadhiwa
katika nyumba ya kulala wageni ya Madevoshini, zilizoko DSm street, Manispaa ya
Moshi, Mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya kusafirishwa kwenda wilayani Same eneo
la Marwa kwa ajili ya kutumikishwa kwenye mashamba ya vitunguu.
Boaz alisema kwamba baada ya kupokea taarifa hizo hatua za
haraka zilichukuliwa kufuatilia taarifa hizo na kukuta watoto 10 (majina
yamehifadhiwa) na baada ya uchunguzi iligundulika kwamba watoto hao
walichukuliwa kutoka kijiji cha Longoi Nguzo Nne, Kikavu chini, Wilaya ya Hai,
mkoani Kilimanjaro kwa lengo la kuwatumikisha katika mashamba ya vitunguu kwa
ujira wa Sh. 1000 kwa kutwa.
Kamanda Boaz, aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni George Benard
massawe( 41), mkazi wa pasua, Lameck Juma Mziray (38), mkazi wa majengo kwa
mtei Moshi, Innocent Marandu (34), mkazi wa Dsm street moshi ambao
wanashikiliwa na jeshi hilo kwa uchunguzi zaidi na baada ya uchunguzi
kukamilika watafikishwa mahakamani.
Kamanda wa polisi alitoa wito kwa wananchi ,wazazi/walezi na
jamii kwa ujumla kushirikiana na jeshi la polisi katika kulinda haki za watoto
na kuwataka kuacha tabia ya kuwatumikisha watoto wadogo, pia aliongezea kuwa
jeshi la polisi lipo macho kuhakikisha linapambana na kudhibiti vitendo kama
hivyo.
Kwa upande mwingine, baadhi ya wananchi wa maeneo hayo, walionyesha
kusikitishwa na kitendo hicho na kusema kuwa mtu mzima hulipwa kuanzia Sh.20000 na zaidi,
kwa hiyo, kitendo cha kuwatumikisha watoto wadogo kwa kuwalipa tuta Sh.1000 ni
unyanyasaji mkubwa na ukiukwaji wa haki za binadamu.
Wananchi hao walilitaka jeshi la polisi mkoani hapo kuchukua
hatua kali kwa watu wanaojihusisha na vitendo kama hivyo vinavyokiuka haki za
watoto katika sekta mbalimbali hapa nchini.(Na Mary Mosha Moshi)
Habari Zingine
Mjulishe Mwenzako
0 MAOINI :