Meya amuonya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro

Posted in
No comments
Monday, February 11, 2013 By danielmjema.blogspot.com



MEYA JAFARI
MEYA wa Mji wa Moshi, Jafari Michael, amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama, kuwa wazi, kama amekuja mkoani hapa kufanya kazi za Serikali au kukiwakilisha Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Meya Michael ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Boma Mbuzi (Chadema), aliyasema hayo juzi kwenye mkutano wa hadhara katika Viwanja vya Pasua Sokoni baada ya kutoridhishwa na mwenendo wa mkuu huyo wa mkoa.


“Nataka niweke wazi suala hili ili kila mtu afahamu ukweli uko wapi. Mimi sina chuki na Gama, mimi Jafari sina ugomvi na Gama, namheshimu kama mkuu wetu wa mkoa, namtambua kama mwakilishi halali wa Rais.

“Ugomvi wangu na yeye ni katika utendaji kwa sababu anaonekana kufanya kazi za chama badala ya kufanya kazi za Serikali.

Akifafanua zaidi, alisema kitendo cha Gama kuingilia kazi za halmashauri pamoja na kupotosha umma, kuwa maazimio ya baraza baadhi yake siyo sahihi kwa sababu lina idadi kubwa ya madiwani wa Chadema, hakiwezi kukubalika kwa sababu anaingilia kazi zisizomhusu.

“Kwa mujibu wa sheria za Serikali za Mitaa, sura ya 190, kifungu cha 87 na sura 188 kifungu cha 47, natambua mamlaka ya Mkuu wa mkoa kama mshauri wa halmashuri zote katika mkoa wake na sheria imekuwa ikikiukwa na mkuu wetu wa mkoa kwani amekuwa kiliagiza baraza badala ya kulishauri,

“Gama ni kada wa CCM na kwa bahati nzuri yeye kisheria ni mjumbe wa mkutano mkuu wa chama chake, inatakiwa afanye kazi za chama katika vikao vyao, akitoka nje anatakiwa kufanya kazi kama mkuu wa mkoa na sio kada wa CCM,” alisema Michael.

Aliwataka viongozi ndani ya CCM kumuiga Rais na Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Jakaya Kikwete ambaye pamoja na kuwa Mwenyekiti wa CCM, hana tabia ya kuchanganya majukumu ya kitaifa na kazi za chama.

Kuhusu suala la Safari ya kwenda Kigali Rwanda na Mombasa Kenya kujifunza usafi iliyokuwa imeandaliwa na Baraza la Madiwani kabla ya kusitishwa kwa kile kilichodaiwa kupingwa na Gama, alimlalamikia mkuu huyo wa mkoa kwa kile alichosema kuwa aliizuia kimakosa.

Pamoja na hayo, alimkata mkuu huyo wa mkoa, kutoa ufafanuzi wa mambo kadhaa yanayokwamisha maendeleo ya mkoa huo, atoe ufafanuzi wa namna ya kudhibiti uharibifu wa mazingira katika Msitu wa Rau na uvunaji mbao katika Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro.

Maeneo mengine ambayo Meya huyo alitaka yatolewe ufafanuzi ni ujenzi wa stendi ya kisasa ya Gangamfumuni ambayo pamoja na taratibu zote kukamilika haijajengwa na ujenzi wa Uwanja wa Memorial ambao umekuwa ukitumika kama soko la mitumba.

Wakati meya huyo akisema hayo, hivi karibuni viongozi wa CCM walipokuwa wakiadhimisha miaka 36 ya kuzaliwa kwa CCM mkoani hapa, walimshutumu meya huyo, kwamba yeye na baadhi ya madiwani, wanamchukia mkuu wa mkoa bila sababu.

chanzo: MTANZANIA

Habari Zingine

0 MAOINI :

Fadhili Athumani



EastAfrica Swahili Blogger, Journalist at Mwanaspoti Kenya, Nairobi Kenya, Call: +254705246475, whatsapp:+255654724337, Email: fadhiliathumani85@gmail.com

Proudly Powered by EAMG .