USIYOYAJUA KUHUSU MAREHEMU JULIUS NYAISANGAH (UNCLE J)
Posted in
No comments
Tuesday, October 22, 2013
By
danielmjema.blogspot.com
Marehemu Nyaisanga (R.IP.) |
Marehemu Julius Nyaisangah, Jina ambalo kwa hakika litabaki kutajwa katika historia ya muziki
Tanzania. Mtangazaji huyu ambaye alitokea Kenya na kuja kujiunga na
Radio Tanzania Dar es Salaam, alikuja na aina mpya ya utangazaji ambayo
ilimfanya apate nafasi ya pekee katika nyoyo za wasikilizaji wa RTD kwa
miaka yote aliyokuweko huko.
Akifahamika kwa wengi waliopenda kusikiliza sauti yake kama Uncle J, Nyaisanga ambaye mwenyewe alisema alitengeneza
staili yake ya utangazaji kwa kumuiga mtangazaji maarufu wa KBC Leonard
Mambo Mbotela aliyejulikana sana kwa kipindi chake 'Je huu ni
uungwana?' alikuja na utangazaji uliochangamsha sana kumsikiliza.
Nyaisanga alikuwa Producer wa mamia ya nyimbo za bendi zilizorekodiwa na
bendi mbalimbali katika studio za RTD miaka ya 80. Nilipata bahati ya
kufanya nae kazi wakati nilienda kurekodi nikiwa katika bendi tatu
tofauti, Orchestra Mambo Bado, Tancut Almasi Orchestra, na Vijana Jazz
Band. Alishauri vizuri na matokeo yake ni nyimbo nyingi zilizopitia
mikononi mwake zingali zinapendwa mpaka leo.
Pamoja na utangazaji, na u producer wa muziki, Nyaisanga alipenda muziki na wanamuziki, alikuwa rafiki wa wanamuziki wengi sana, alikuwa na tabia ya kutembelea bendi zinapopiga na aliweza hata kutembelea bendi nne au tano kwa usiku mmoja.
Na hasa kama bendi iko katika ratiba ya
kurekodiwa. Aliwahi hata kufika Iringa kutembelea tancut Almasi
Orchestra kabla ya kurekodi toleo lao lililokuwa naule wimbo usiochosha
Masafa Marefu.
Nyaisanga alipita kwenye bendi kadhaa kututaarifu kuhusu
kuanza kwa radio mpya ambayo ingekuwa katika masafa ya FM, na ndipo muda
si mrefu Radio One ikaingia hewani wakati huo ikiwa pale katika jengo
la NASACO ambalo lilikuja kuungua na baada ya kukarabatiwa sasa linaitwa
Waterfront.
Pia akiwa Radio One Nyaisanga aliendelea kuwa Nyaisanga,
japo sera za Radio One hakika zilikuwa tofauti na zile za RTD, lakini
pia huko mchango wake katika muziki ulikuwa mkubwa sana.
Hatimaye
Nyaisanga alihamia Abood Radio Morogoro ambako amekuweko mpaka hatimae
usiku wa kuamkia leo 20 October 2013, umauti umemkuta katika hospitali
ya Mazimbu Morogoro kutokana na kusumbuliwa kwa muda mrefu na Kisukari.
MUNGU AMLAZE PEMA PEPONI JULIUS NYAISANGA (UNCLE J)
Habari Zingine
Mjulishe Mwenzako
0 MAOINI :