Nelson Mandela kuzikwa Desemba 15
Posted in
No comments
Saturday, December 7, 2013
By
danielmjema.blogspot.com
SIKU
moja baada ya kifo cha Rais wa kwanza mweusi wa Afrika Kusini, Mzee
Nelson Mandela (95), mazishi yake yanatarajiwa kufanyika wiki moja
kuanzia sasa, Desemba 15, siku ya Jumapili.
Mazishi hayo ya kihistoria na ya aina yake, yatafanyika katika kijiji
chake cha Qunu, mahala alipopachagua mwenyewe kabla ya kifo chake.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Rais wa Afrika Kusini,
Jacob Zuma, Mzee Madiba atazikwa katika eneo hilo la Mashariki ya Cape
kwa heshima zote.
Zuma alisema mazishi ya kitaifa, ikiwamo utoaji wa heshima za mwisho,
yatafanyika jijini Pretoria ambapo baadaye mwili wake utasafirishwa
kwenda Mkoa wa Cape Mashariki hadi katika Kijiji cha Qunu ambako ndiko
Mzee Madiba alipozaliwa na kukulia.
Aidha, taarifa hiyo ilieleza kuwa Mzee Madiba atazikwa kwa sherehe maalumu za kimila karibu na makaburi ya watoto wake watatu.Kutokana na msiba huo ulioikumba dunia, wakuu wa nchi mbalimbali
duniani, akiwemo Rais wa Marekani, Barack Obama, Oprah Winfrey na
Hillary Clinton wanatarajiwa kuhudhuria mazishi hayo mbali ya viongozi
wengine kutuma salamu za rambirambi kwa Rais Zuma na kwa familia ya Mzee
Madiba.
Viongozi duniani wanena
Miongoni mwa marais waliotuma salamu za rambirambi kwa Rais Zuma na
kwa mjane wa Mzee Madiba, Graca Machel, wanafamilia wote na wananchi
wote wa Afrika Kusini ni pamoja na Jakaya Kikwete wa Tanzania ambaye pia
ametangaza siku tatu za maombolezo kuanzia jana hadi Desemba 8 na
kuagiza bendera kupepea nusu mlingoti kwa siku hizo.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Kin Moon alisema Mandela
alikuwa kielelezo cha Umoja wa Mataifa kwani alikuwa mtu wa heshima na
mtetezi wa haki za binadamu, aliyepinga ubaguzi wa rangi na mpigania
usawa.
“Kwa niaba ya Umoja wa Mataifa, natoa rambirambi zangu kwa watu wa
Afrika Kusini na hasa kwa familia ya Nelson Mandela na wapendwa,”
alisema.
Aidha, Moon alieleza kuwa inashangaza, kuona Mandela alitoka
kizuizini bila uadui baada ya kifungo cha miaka 27, ambapo nia yake
ilikuwa kujenga nchi yake katika misingi bora kwa kutumia akili.
Salamu za Rais Kikwete kwa Zuma
Rais Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Rais Zuma, wanafamilia na
wananchi wote wa Afrika Kusini kutokana na kifo cha Mzee Mandela.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mwandishi wa habari wa rais
msaidizi, Ikulu Premi Kibanga, Rais Kikwete ametangaza siku tatu za
maombolezo kuanzia jana Desemba 6 hadi 8 mwaka huu.Aidha, Rais Kikwete alisema kuwa katika siku hizo bendera zote zitapepea nusu mlingoti.
Rais Kikwete alisema kuwa msiba huo ni wa bara zima la Afrika na dunia.“Afrika Kusini, Afrika na dunia kwa ujumla imepoteza mtu mashuhuri na
shujaa mkubwa wa karne ya 20 na 21. Tunaelewa machungu waliyonayo
wananchi wa Afrika Kusini kwa kupoteza kiongozi shupavu, jasiri,
mwanamapinduzi na mstahamilivu,” alisema.
Rais Kikwete alimuelezea Mzee Mandela kuwa ni kielelezo cha aina
yake kwa wanadamu kwa moyo wake wa kusamehe, huruma na upendo
uliomuwezesha kuwaunganisha wananchi wa Afrika Kusini kuwa taifa moja
baada ya kipindi kirefu cha mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi.
“Mandela ni mfano bora kwa wanadamu, wa jinsi binadamu muungwana
anavyopaswa kuwa. Ni wajibu wa wana Afrika Kusini, Afrika na dunia kwa
jumla kuiga mfano wake, hasa moyo wake wa uzalendo, kujitolea hata
maisha yake kwa ajili yake na wananchi wenzake.”
Alisema ni muhimu kumuombea kwa Mwenyezi Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi.
Kwa upande wake Mkuu wa Idhaa za Kiafrika katika DW, Claus Stäcker
alisema kuwa vyombo vya habari na wanasiasa duniani kote wanaendelea
kushindana katika kuonyesha heshima zao kwa Mandela, ambaye yeye
mwenyewe hakupenda kuchukuliwa kama Mungu.
Stäcker alisema Mandela hakuwa mtakatifu, hata ingawa hivyo ndivyo
vyombo vya habari vinavyomwelezea. Kila kichwa cha habari kinamfanya
aonekane kama mtu aliyefanya maajabu na hasa kuonekana kama kuiabudu
sanamu.
“Mandela mwenyewe hakupenda kuabudiwa. Alikuwa akikubali tu shingo
upande barabara, shule na taasisi kuitwa jina lake, kuruhusu sanamu za
shaba na majumba ya makumbusho ya Mandela kujengwa, mtindo ambao bila
shaka utaendelea kukua,” alibainisha Stäcker.
Jijini Dar es Salaam, vilio, simanzi na majonzi vilitawala katika
Ofisi za Ubalozi wa Afrika Kusini uliopo nchini baada ya raia wa mataifa
mbalimbali wakiwemo Waafrika Kusini wanaoishi nchini, kufika kwa ajili
ya kutoa pole kutokana na kifo cha Mzee Mandela.
Raia hao ambao wengi ni wa kigeni walifika katika ubalozi huo kuanzia
majira ya saa moja asubuhi, huku wakibeba mashada ya maua na kuyaweka
katika picha kubwa ya Mandela iliyowekwa mbele ya ofisi za kuingilia za
ubalozi huo.
Raia wa Canada anayeishi hapa nchini aliyejitambulisha kwa jina moja
la Jeff, alisema ameguswa na kifo hicho kutokana na Mzee Mandela kuwa
mfano bora kwa jamii hasa katika harakati zake za kupinga ubaguzi wa
rangi.“Nimeamua kuambatana na familia yangu kuja kutoa pole kwa kifo hicho
kimetugusa sana kwani tumekuwa tukimuangalia Mandela kama mfano wa
kuigwa kwa dunia nzima,” alisema.
Akizungumzia kifo hicho, Balozi wa Afrika Kusini nchini, Thanduyise
Henry Chiliza alisema ni huzuni kubwa na majuto kuwajulisha kuwa rais wa
zamani na nembo ya kitaifa, Nelson Rolihlahla Mandela, amefariki dunia
juzi Desemba 5, mwaka huu, majira ya saa 2:50 usiku akiwa na umri wa
miaka 95.
“Ingawa sisi tulijua kwamba siku hii itakuja, lakini hakuna kitu
kinachoweza kupunguza hisia zetu na hasara kubwa tuliyopata na ya kudumu
kwa kumpoteza kiongozi huyo,” alisema.
Alisema kutokana na msiba huo bendera ya taifa hilo itapepea nusu mlingoti hadi mazishi ya Mzee Mandela yatakapofanyika.“Kitabu cha maombolezo kimefunguliwa katika ubalozi wetu plot 1338/9,
barabara ya Mwaya, Masaki, Dar es Salaam kuanzia Jumatatu hadi Alhamisi
saa 3:30 hadi saa 9:30 na Ijumaa saa 3:30 hadi saa 6:30 mchana kasoro
siku za sikukuu,” alisema.
Chiliza alisema Serikali ya Afrika Kusini inaendelea na mipango ya
mazishi na Waafrika Kusini kila pembe ya dunia watajulishwa suala hilo.
Maisha ya Mandela
Mandela alikuwa mtu aliyezaliwa kuwa kiongozi.Kama rafiki yake waliyefungwa naye pamoja, Ahmed Kathrada, alivyosema
hivi karibuni, Mandela alizaliwa katika familia ya kifalme na ilikuwa
kawaida kwake kuwa alizaliwa kuwa kiongozi.
Mandela alijibeba vyema sana alipokuwa kiongozi wa chama cha ANC na
kwamba hakuna hata nusu ya imani yake iliwahi kumuondoka miaka yote 27
aliyokuwa gerezani.Ingawa Mandela alijitaja mwenyewe kuwa kama sehemu tu ya uongozi wa
ANC, hapakuwa na shaka kuwa alikuwa kiongozi mkuu wa chama hicho kwa
kizazi chake wakati huo nchini Afrika Kusini.
Kwa dunia nzima Mandela alikuwa ishara ya mambo mengi, sio kiongozi
tu, lakini mfano wa viongozi ambao dunia inastahili kuwa nao enzi hizo.
Wengi wanamfahamu Mandela kwa kuwa na moyo mwepesi wa kusamehe na
wengi wanamkumbuka hivyo kwani baadhi walimshangaa sana miaka ya tisini,
aliposema kuwa hana chuki na mtu na kuwa amewasamehe waliomtendea ubaya
na hata kumfunga.
Alizaliwa mwaka 1918, katika Rolihlahla Dalibhunga, na kulelewa katika Kijiji cha Mvezo Mashariki mwa Mkoa wa Cape.Alikuwa na ndugu zake 13 katika familia iliyokuwa na uhusiano wa karibu na familia ya kifalme ya Thembu.
Mandela alienziwa na wengi kwa sababu ya vita aliyopigana dhidi ya utawala wa wazungu.Baba yake alifariki Mandela akiwa na miaka tisa. Alimtaja baba yake kama mtu mkali mwenye kutaka watu kufuata maadili mema.
Lakini alimsifu sana baba yake kwa kumsisitizia kuwa na maadili mema kwani yeye ndiye alimfanya kuwa mtu mwema maishani.Ilikua muhimu kwake kupata elimu. Na hivyo akasomea katika shule ya
kimethodisti na kisha mwaka 1939 akaenda katika Chuo Kikuu cha Fort
Hare.
MAISHA YAKE KWA UFUPI
1943: Alijiunga na chama cha ANC.
1956: Alifunguliwa kesi ya uhaini, lakini baada ya miaka minne ikatupiliwa mbali.
1962: Alikamatwa na kushitakiwa kwa kosa la uchochezi na kufungwa jela miaka mitano.
1964: Alishitakiwa kwa kosa la kuhujumu serikali na kufungwa maisha jela.
1990: Aliachiliwa kutoka gerezani.
1993: Alishinda tuzo ya Amani ya Nobel.
1994: Alichaguliwa kuwa rais wa kwanza mweusi Afrika Kusini.
1999: Aling’atuka madarakani.
2001: Aligundulika kuwa na saratani ya tezi kibofu.
2004: Alistaafu.
2005: Alitangaza kuwa mwanawe alifariki kwa maradhi ya ukimwi.
Habari Zingine
Mjulishe Mwenzako
0 MAOINI :