WAZIRI MUKANGARA MGENI RASMI KILIMANJARO MARATHON
Posted in
Michezo
No comments
Sunday, February 23, 2014
By
danielmjema.blogspot.com
Mhe. Dk. Fenella Mukangara |
Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Mhe. Dk. Fenella
Mukangara anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye mbio mbio za 12 za Kilimanjaro
Marathon ambazo zinatarajiwa kufanyika Jumapili ijayo tarehe 2 Machi, 2014
mjini Moshi.
Aggrey Marealle, Mkurugenzi Mkuu wa Executive Solutions, waratibu
wa mbio hizo alisema jana kwamba Dr. Mukangara amekubali kuwa mgeni rasmi na
atahuduria sherehe ya utoaji zawadi ambapo atatoa zawadi kwa washindi kumi wa
mbio defu za kilomita 42 maarufu kama Full Marathon kwa wanaume na wanawake.
Aggrey Marealle |
“Uwepo
wa waziri ni ishara ya uungaji mkono tukio hili na ameeleza kufurahishwa kwake
na maandalizi ya hali ya juu ya Kilimanjaro Marathon. Dk. Mukangara ameeleza
mara kadhaa kwamba serikali inaunga mkono Kilimanjaro Marathon kwa kutambua
mchango wake michezo, utalii na uchumi,” alisema Marealle.
Marealle aliongeza kwamba baada ya sherehe ya utoaji zawadi
Waziri ataungana na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro na mpenda michezo Mhe. Leonidas
Gama, wawakilishi wa wadhamini na watu wengine mashuhuri kwenye mlo maalum wa mchana uliodhaminiwa na Kibo Palace Hotel.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro binafsi na kupitia ofisi yake amekuwa muungaji
mkono wa Kilimanjaro Marathon na amekuwa akifurahia kukaribisha maelfu ya watu
wanaokuja Moshi kutoka mataifa mbalimbali.
John Addison, Mkurugenzi Mkuu wa Wild Frontiers, waandaaji
wa mbio hizo alisema “mbio za mwaka huu zimesheheeni motisha mbalimbali za
kuvutia ili kuongeza idadi ya washiriki. Washindi wa kwanza kwenye mbio ndefu
za kilomita 42 (Kilimanjaro Premium Lager Marathon) wanawake kwa wanaume
watajinyakulia kiasi cha shilingi milioni 4 kila mmoja, shilingi milioni mbili
kwa washindi wa pili na shilingi milioni 1 kwa washindi wa tatu. Washindi wa
kwanza kwenye mbio ndefu za nusu
marathon (km 21) wanawake kwa wanaume watajinyakulia kiasi cha shilingi milioni
2 kila mmoja, shilingi milioni 1 kwa washindi wa pili na shilingi 500,000 kwa
washindi wa tatu.
Waandaaji John Addison wa Wild Frontiers, Mwesiga Kyaruzi wa Executive Solutions na Debbie Harrison |
Addison aliongeza kuwa medali na t-shirt zitatolewa kwa
wanariadha 500 wa kwanza kumaliza mbio za kilomita 42, wanariadha 2,200 wa
kwanza kumaliza mbio za nusu marathon na wanariadha 80 wa kwanza kumaliza mbio
za walemavu. Washiriki 3,000 wa kwanza
kumaliza mbio za kujifurahisha za Vodacom 5km Fun Run watapewa t-shirts baada
ya kumaliza mbio na watapata fursa ya kujishindia zawadi mbalimbali za kuvutia
kupitia droo.
Mbio hizi zinaratibiwa na kwa kushirikiana na Riadha
Tanzania, Chama cha Riadha Mkoa wa Kilimanjaro na Kilimanjaro Marathon Club huku
zikidhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager, Vodacom Tanzania, GAPCO, Simba
Cement, KK Security, Keys Hotel, TPC Sugar, TanzaniteOne, CMC Automobiles Ltd,
Kibo Palace Hotel, RwandAir, FNB Tanzania, UNFPA na Kilimanjaro Water.
Habari Zingine
Mjulishe Mwenzako
0 MAOINI :