Miaka 53 Uhuru...Happy Birth Day Tanzania!

Posted in
No comments
Tuesday, December 9, 2014 By danielmjema.blogspot.com

Dar es Salaam. Tanzania inaadhimisha miaka 53 ya Uhuru leo huku wananchi wa kada mbalimbali wakiielezea siku hii kuwa haina uhalisia wa maisha ya Watanzania.
Rais Jakaya Kikwete atakuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo itakayofanyika katika Uwanja wa Taifa, ambako atakagua gwaride la vikosi vya majeshi ya ulinzi na usalama na baadaye kuwatunuku nishani za heshima kwa watu mbalimbali waliotumikia Taifa.
Katika maadhimisho hayo, pia kutakuwa na michezo ya halaiki, sarakasi, ngoma za asili kutoka katika baadhi ya mikoa ya Tanzania Bara na Zanzibar. Kaulimbiu ya mwaka huu ni; “Miaka 53 ya uhuru; ingia katika historia ya nchi yetu; jitokeze kuipigia kura Katiba Inayopendekezwa.”
Wakati hayo yakifanyika, wadau mbalimbali wameielezea miaka 53 ya Uhuru kwa mtazamo tofauti.
Mkuu wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere ambacho pia kinatimiza miaka 53 leo, Profesa Shadrack Mwakalila alisema sherehe hizo zinafanyika wakati nchi inatajwa kukithiri kwa vitendo vya ukosefu wa maadili kwa viongozi.
Alisema hali hiyo imechangiwa kwa kiasi kikubwa na ukosefu wa mafunzo na elimu ya maadili kwa viongozi kama ilivyokuwa siku zilizopita, hivyo kuna haja ya mafunzo hayo kurudishwa.
Alisema miaka ya 1971 hadi 1991 wakati chuo hicho kikiitwa Chuo cha Chama Kivukoni, kilikuwa kinatoa mafunzo ya maadili na uongozi kwa watendaji wote wa Serikali kabla hawajaenda kulitumikia Taifa, hali ambayo sasa haipo na ndiyo inayochangia kinachotokea sasa.
Profesa Gaudence Mpangala wa Chuo Kikuu cha Ruaha, alisema tofauti na mwaka 1972 hadi 1980 wakati elimu iliyokuwa inatolewa ilikuwa na mwelekeo, kwa sasa kiwango kimeshuka kwa kiasi kikubwa.Alisema kuna sababu mbalimbali za kushuka, ikiwamo ukosefu wa walimu, motisha kwa walimu na zana za kufundishia.
Profesa Mpangala alisema pamoja na sasa kuwapo vyuo vingi, tatizo kubwa ni ukosefu wa ajira... “Kila mwaka vyuo vinamwaga wahitimu, lakini hawana kazi. Uchumi wa Tanzania hauwezi kuwaandaa wasomi kuingia kwenye soko la ushindani… tatizo siasa zinaingizwa kwenye elimu,” alisema.
Mtaalamu wa maendeleo na siasa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Dk Idd Makombe alisema miaka 53 ni mingi na kama nchi ilitakiwa kuwa imepiga hatua zaidi kimaendeleo badala ya kuendelea kuwa maskini duniani.
Alisema kuna nchi ambazo kipindi Tanzania inapata uhuru zilikuwa sawa nayo lakini leo zimepiga hatua.

Habari Zingine

0 MAOINI :

Fadhili Athumani



EastAfrica Swahili Blogger, Journalist at Mwanaspoti Kenya, Nairobi Kenya, Call: +254705246475, whatsapp:+255654724337, Email: fadhiliathumani85@gmail.com

Proudly Powered by EAMG .