TANZANIA: OLDUVAI GORGE IPO TANZANIA SIO KENYA

No comments
Monday, February 29, 2016 By danielmjema.blogspot.com

BODI ya Utalii Tanzania (TTB) imekuwa ikifuatilia kwa makini majadiliano yanayoendelea katika mitandao mbalimbali ya kijamii kufuatia video iliyotumwa katika YouTube https://www.youtube.com/watch?=iveX49WE7fw na imekuwa ikisambazwa kupitia njia mbalimbali za habari ikimuonesha mtu mmoja kutoka nchi jirani akisema kuwa Olduvai Gorge ambayo kimsingi iko Tanzania kwamba iko Kenya.

Video hii imeibua majadiliano katika mitandao ya kijamii baina ya watanzania na watu wengine ambao wanaitakia mema Tanzania na wanaoelewa vizuri kuwa Olduvai Gorge iko Tanzania.

Bodi ya Utalii Tanzania kama taasisi ya Umma yenye jukumu la kuvitangaza vivutio vyetu vya utalii imeshtushwa na video hii iliyojaa upotoshwaji mkubwa ambao tunaamini mbali ya malengo mengine inalenga kuchafua kazi nzuri ambayo imekuwa ikifanywa na Bodi kwa kushirikiana na wadau wengine katika kutamgaza vivutio vya utalii vya Tanzania ikiwemo Olduvai Gorge.

Tunapenda kuchukua fursa hii kupinga vikali upotoshwaji huu uliofanywa na mtu huyo wakati akihutubia mkutano amabao tumeambiwa ulikuwa ni wa Vijana wa Umoja wa Mataifa uliofanyika Amerika mwezi Agosti mwaka jana. Tunapenda dunia ifahamu kuwa kama ilivyo kwa Mlima Kilimanjaro, Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Zanzibar n.k Olduvai Gorge mahali panapoaminika kuwa ndipo binadamu wa kwanza duniani aliishi na ambako Dr. Louis na Mary Leakey waligundua fuvu la binadamu huyo wa kale anayesadikiwa kuishi miaka takribani milioni 2 iliyopita iko pia Tanzania na si mahali pengine popote duniani. Eneo hili la Olduvai Gorge liko katika bonde la ufa katikati ya bonde la Ngorongoro na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti mkoani Manyara nchini Tanzania.

Tunatoa wito kwa watanzania mahali popote walipo kuendelea kuunga mkono juhudi za Bodi ya Utalii Tanzania za kuitangaza Tanzania na vivutio vyake vya Utalii kwa kujibu na kusahihisha papo hapo bila woga mara tu taarifa ya upotoshaji kuhusu nchi yetu inapotolewa iwe ni kwenye mikutano ya ndani ya nchi au ya Kimataifa. Tunaamini kuwa ni jukumu la kila mtanzania kuitangaza Tanzania na vivutio vyake vya Utalii badala ya kuiachia TTB kazi hii peke yake. 

Yawezekana katika mkutano huo wa vijana ambao mjumbe huyo wa nchi jirani alipata fursa ya kuzungumza na kufanya upotoshaji huzo, wajumbe wa Tanzania pia walikuwepo ambao wangweza kukosoa upotoshaji huo papo hapo na kuelezea ukweli na usahihi wa mahali ilipo Olduvai Gorge.

Imetolewa na:
Ofisi ya Uhusiano

BODI YA UTALII TANZANIA.

Habari Zingine

0 MAOINI :

Fadhili Athumani



EastAfrica Swahili Blogger, Journalist at Mwanaspoti Kenya, Nairobi Kenya, Call: +254705246475, whatsapp:+255654724337, Email: fadhiliathumani85@gmail.com

Proudly Powered by EAMG .