MICHEZO: KIKOSI CHA DHAHABU CHA UFARANSA KINACHOTESA KWENYE UKOCHA

Posted in
No comments
Monday, March 7, 2016 By danielmjema.blogspot.com

Zinedine Zidane, Thiery Henry, Masseile Desailly na Patrick Vieira
KATIKA Dimba la Stade de France, mechi ya fainali ya Kombe la Dunia, "Samba Boys" walikula 3-0 mbele ya mafundi hawa wa Ufaransa, kikosi ambacho kwangu ni kikosi bora kuwahi kutokea nchini Ufaransa. Ni  kikosi kilichoishtua dunia baada ya kutwaa Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza katika historia ya Ufaransa. Ilitokea hivyo mwaka 1998 katika ardhi ya nyumbani. 

Baadaye mastaa wengi wa kikosi kile kilichoundwa cha Claude Makelele, Thiery Henry, Zinadine Zidane, Patrick Vieira, Laurent Blanc, Manuel Petit, Nahodha Didier Deschamps, Lionel Charbonnier, Alain Boghossian, Bernard Lama na wengineo, wamegeukia kazi ya ukocha na sasa wanatamba katika klabu mbalimbali duniani.

THIERRY HENRY

Staa wa zamani wa Arsenal ambaye alikuwepo katika kikosi cha Ufaransa cha mwaka 1998 lakini akitokea katika klabu ya Monaco. Henry ambaye baada ya michuano hiyo alitua Juventus ya Ufaransa ambayo alidumu kwa msimu mmoja ilipomuuza kwenda Arsenal kuwa staa. Kwa sasa anaendelea kujichua katika timu ya vijana ya Arsenal kama mmoja kati ya makocha.

ZINEDINE ZIDANE

Nyota mkubwa zaidi katika kikosi kile cha Ufaransa ambaye alitupia mabao mawili katika ushindi wa mabao 3-0 pambano la fainali dhidi ya Brazil Stade de France. Zidane hakutabiriwa kuwa kocha kutokana na tabia yake ya upole lakini alianza kazi hiyo taratibu katika timu ya vijana ya Real Madrid ambayo alistaafia soka mara baada ya kumalizika kwa michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2006

Baada ya kusota katika timu ya vijana ya Madrid, Zidane amepandishwa cheo na kuwa kocha mkuu wa Madrid akichukua nafasi ya kocha aliyetimuliwa klabuni hapo Rafa Benitez. Haijaeleweka kama Zidane atakuwa kocha wa kudumu ifikapo mwishoni mwa msimu huu.

PATRICK VIEIRA

Staa wa zamani wa Arsenal ndiye alipiga pasi ya bao la mwisho la Ufaransa katika pambano dhidi ya Brazil kwenda kwa Manuel Petit ambaye alikuwa akicheza naye timu moja Arsenal.Vieira alianza kujifunza ukocha akiwa Manchester City na baadaye kuibukia kuwa kocha wa vijana wa timu hiyo. 

Hata hivyo, Novemba 9,2015 Vieira alichaguliwa kuwa kocha mkuu wa klabu ya New York City FC ya Marekani ambayo pia inamilikiwa na matajiri wa Manchester City. Inasemekana Vieira anaandaliwa kuwa mrithi wa kocha mtarajiwa wa Man City,Pep Guardiola. Pia Arsenal wanamtaja kuwa miongoni mwa watu wanaoweza kumrithi Arsene Wenger

LAURENT BLANC

Mlinzi nyota wa Ufaransa ambaye alilikosa pambano la fainali baada ya kupewa kadi mbili za njano mechi ya nusu fainali dhidi ya Croatia. Kwa sasa Blanc ni kocha wa kikosi cha PSG ambacho kimekuwa kikisumbua barani Ulaya baada ya kufanikiwa kutawala katika Ligi Kuu Ufaransa. 

Mara baada ya kumaliza maisha yake ya soka alianza kazi ya ukocha katika klabu ya Bordeaux ya kwao Ufaransa mwaka 2007, huku akitwaa ubingwa wa Ufaransa msimu wa 2008–09. Baada ya kuondoka mwaka 2010 aliteuliwa kuwa kocha wa timu ya taifa ya Ufaransa mwaka huo akichukua nafasi ya Kocha Raymond Domenech aliyekuwa amechemsha katika michuano ya Kombe la Dunia 2010.

Aliifundisha timu hiyo mpaka mwaka 2012 alipofanikiwa kuifikisha Ufaransa katika robo fainali za michuano ya Euro 2012.Mwaka 2013 ndipo alipoajiriwa na PSG huku akitawala sana soka la ndani.
DIDIER DESCHAMPS

Nahodha wa kikosi kile cha Ufaransa ambaye pia anaingia katika historia ya kuwa nahodha wa pili kutwaa mataji ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, Kombe la Dunia na Kombe la Euro. Mara baada ya kuachana na soka, Deschamps aliteuliwa kuwa kocha wa kikosi cha Monaco huku akitwaa Kombe la Ligi ya nchini hiyo mwaka 2003. 

Pia akaipeleka katika fainali zao za kwanza la Ligi ya Mabingwa ambayo hata hivyo walipoteza baada ya kupigwa 3-0 na Porto mwaka 2004. Baada ya kukorofishana na Rais wa klabu hiyo alijiuzulu lakini mwaka 2006 akaibukia kwa wababe wa Italia Juventus ambao walikuwa wameshushwa daraja kutokana na kashfa ya kupanga matokeo.

Baadaye alifanikiwa kuipandisha Ligi Kuu timu hiyo lakini kabla hajaiongoza katika mechi yoyote ya Ligi Kuu alikorofishana na mabosi wa Juventus na kuamua kujiuzulu. Baadaye alirudi Marseille ambapo aliwapa taji lao la kwanza la ubingwa wa Ligi baada ya miaka 18. 

Julai 2012 alichaguliwa kuwa kocha wa timu ya taifa ya Ufaransa akirithi mikoba ya mchezaji mwenzake wa kikosi cha Ufaransa 1998,Laurent Blanc. Mpaka sasa Deschamps ni kocha wa timu ya taifa ya Ufaransa na anatazamiwa kuiongoza katika michuano ya Euro 2016.

LIONEL CHARBONNIER

Lionel Andre Michel Charbonnier alikuwa kipa namba tatu wa kikosi kile cha Ufaransa baada ya Fabien Barthez na Bernard Lama. Baada ya kuachana na soka Charbonnier aliibukia katika kazi ya ukocha katika klabu ya Atjeh United ya Ligi Kuu ya Indonesia. Baadaye aliibukia katika klabu za Stade Poitevin, FC Sens, timu ya Tahiti chini ya umri wa miaka 20. Kwa sasa ni mkurugenzi wa ufundi wa timu ya taifa ya Indonesia.

ALAIN BOGHOSSIAN
Kiungo aliyekwenda katika fainali zile huku akikumbukwa kwa kuingia katika kipindi cha pili cha pambano la fainali dhidi ya Brazil akichukua nafasi ya kiungo,Christian Karembeu. Kwa sasa Boghossian ni kocha msaidizi katika kikosi cha timu ya taifa ya Brazil akimsaidia kazi rafiki yake, Didier Deschamps ambaye walicheza wote katika kikosi kile.

BERNARD LAMA

Kipa namba mbili wa kikosi kile ambaye kama ilivyo kwa Charbonnier naye hakudaka hata mechi moja.Julai 21, 2006 Lama alichaguliwa kuwa kocha mkuu katika kikosi cha timu ya taifa ya Kenya. Hata hivyo,katika mechi yake ya kwanza tu alipigwa na Eritrea mnamo Septemba 2,2006 katika pambano la kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika. Aliachia ngazi miezi miwili tu baadaye akilalamikia ubabaishaji wa Shirikisho la Soka la Kenya. Nafasi yake ilichukuliwa na Tom Olaba.

Habari Zingine

0 MAOINI :

Fadhili Athumani



EastAfrica Swahili Blogger, Journalist at Mwanaspoti Kenya, Nairobi Kenya, Call: +254705246475, whatsapp:+255654724337, Email: fadhiliathumani85@gmail.com

Proudly Powered by EAMG .