TANZANIA: RAIS DKT MAGUFULI AMTUMIA SALAMU ZA RAMBIRAMBI, RAIS MSTAAFU, DKT KIKWETE
Posted in
afrika mashariki
No comments
Tuesday, March 1, 2016
By
danielmjema.blogspot.com
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli
amemtumia salamu za rambirambi Rais Mstaafu wa awamu ya nne Dkt. Jakaya
Mrisho Kikwete kufuatia kifo cha Kaka yake Mzee Selemani Mrisho Kikwete,
kilichotokea leo asubuhi nchini India.
Mzee Selemani Mrisho Kikwete alikuwa nchini India kwa matibabu. Katika salamu zake Rais Magufuli amesema amepokea kwa mshituko
taarifa za kifo cha Mzee Selemani Mrisho Kikwete na amesema anaungana na
familia ya Rais Mstaafu Kikwete kuombeleza kifo cha mtu muhimu kwa
familia hiyo.
"Napenda kukupa pole nyingi wewe Mheshimiwa Rais Mstaafu
Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, familia yenu yote, ndugu jamaa na marafiki
kwa kuondokewa na mtu muhimu katika familia, natambua uchungu mkubwa
mlionao lakini nawaomba muwe na uvumilivu na ustahimilivu katika kipindi
hiki kigumu" Alisema Rais Magufuli.
Dkt. Magufuli amemuombea Marehemu Mzee Selemani Mrisho Kikwete apumzishwe mahali pema peponi, Amina. Inna lillahi wa inna ilayhi raji'un.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU.
Arusha
01 Machi, 2016
Habari Zingine
Mjulishe Mwenzako
0 MAOINI :