KENYATTA: KENYA ITATIMIZA MASHARTI YA WADA

No comments
Tuesday, April 12, 2016 By danielmjema.blogspot.com

Kenya itatimiza muda wa mwisho wa mwezi Mei kufuata mfumo wa shirika linalopambana na matumizi ya madawa ya kuongeza nguvu misuli, WADA na kuepuka vikwazo. Vikwazo hivyo ni pamoja na kupigwa marufuku kushiriki katika michezo ya Olimpiki ya Rio. 

Akizungumza katika hafla ya chai ya asubuhi aliyowaandalia wanariadha watakaoshiriki katika mbio ndefu, marathon na mbio za dunia za nusu marathon ikulu mjini Nairobi, Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta amesema serikali yake imeupa mswada huo umuhimu na anaufuatilia kwa karibu.

Ifikapo mwishoni mwa juma, mswada wa kupambana na madawa hayo, utakuwa umepitishwa na bunge na nitautia saini kuwa sheria ili kusiwe na kisingizio cha kuinyima timu yetu kushiriki katika michezo ya Olimpiki mjini Rio de Janeiro mwezi Agusti, amesema.

 "Tunafahamu kuna watu wanaotafuta visingizio kuhakikisha kwamba Kenya haishiriki katika Olimpiki. Hatutawapa nafasi hiyo" alinukuliwa akisema katika taarifa rasmi ya serikali.


Kenya imepatiwa muda wa nyongeza wa mwezi mmoja hadi Aprili 7 kufuata mfumo wa WADA ama itakabiliwa na vikwazo ambavyo ni pamoja na kupigwa marufuku kushiriki michezo ya Olimpiki ya Rio mwaka huu.




Kauli ya Rais Kenyatta imekuja huku kukiwa na habari njema kwa wanariadha wa Kenya, watakaoshiriki mbio za Olimpiki mjini Rio de Janeiro, nchini Brazil, baada ya WADA, kuiongezea Kenya muda wa kutunga Sheria za kukabiliana na matumizi ya Dawa za kusisimua misuli michezoni.

Kenya wiki iliyopita, ilikosa kutimiza muda wa mwisho wa pili uliowekwa mwaka huu, wakati kamati huru ya kuangalia uzingatiaji wa sheria hizo iliamua kuwa mpango wa Kenya wa kupambana na dawa za kuongeza misuli nguvu hauzingatii sheria za kimataifa.

Ikiwa Kenya haitapitisha sheria ya kufanya iwe uhalifu matumizi ya dawa hizo zilizopigwa marufuku michezoni na kuidhinisha rasmi sheria za shirika lake jipya la kitaifa la kupambana na dawa hizo ifikapo mwezi ujao, kamati ya mapitio itaiambia bodi ya WADA kuitangaza Kenya kuwa nchi isiyozingatia viwango hivyo.
Hatua hiyo imewatia moyo maafisa wa Kenya pamoja na wanariadha akiwemo bingwa wa dunia katika mchezo wa kurusha mkuki Julius Yego ambaye amesema sasa ni jukumu la serikali kuiharakisha sheria hiyo. 

"Nataka kusema serikali inapaswa kuchukua hatua ya haraka na kupitisha mswada huo ili kila kitu kiende sawa. Wakati tukijiandaa, hatutaki hali ambayo labda baadhi ya watu watasema Kenya itapigwa marufuku. Nataka wakati nikishiriki mashindanoni, kila mtu afahamu kuwa Kenya inazingatia sheria na sio kama baadhi ya nchi ambako kumekuwa na matatizo ya kutozingazia sheria hizo"

Habari Zingine

0 MAOINI :

Fadhili Athumani



EastAfrica Swahili Blogger, Journalist at Mwanaspoti Kenya, Nairobi Kenya, Call: +254705246475, whatsapp:+255654724337, Email: fadhiliathumani85@gmail.com

Proudly Powered by EAMG .