Nawaza kwa Sauti: Leo Nimemkumbuka Shujaa Patrice Lumumba
Posted in
Jicho la Habari
No comments
Sunday, May 29, 2016
By
danielmjema.blogspot.com
Ni barua ambayo siku ya kwanza nilipoisoma miaka kadhaa huko nyuma ilinitoa machozi sana. Katika barua ile alimwambia mke na watoto wake kuwa hana uhakika kama barua ile itawafikia lakini pia hana uhakika kama ataweza kuwaona tena.
Juu ya yote alieleza kuwa anajisikia fahari sana kwa kuwa hayuko tayari kuwa kibaraka wa kikoloni na kuwasaliti wananchi wa kongo kwa jambo lolote lile,yuko tayari kufa ili mradi anasimamia jambo sahihi kwa manufaa ya wengi. Barua hii inanikumbusha maneno ya Emiliono Zambata,kamanda wa jeshi na mwanamapinduzi wa mexico aliyesema:
”Ni bora kufa umesimama kuliko kuishi huku umepiga magoti”.Ghafla nikakumbuka maneno ya mwanaharakati mweusi wa marekani, Martin Luther Jr aliposema-“Kama haujapata jambo ambalo uko tayari kutoa uhai wako kwa hilo basi haufai kuendelea kuishi”,maneno haya makali yakanipeleka kwa Steven Bikko aliyesema-“Ni bora kufa kwa wazo litakaloishi kuliko kuishi kwa wazo litakalokufa”
Watu hawa hawakumaanisha kuwa hawapendi kuishi na wanapenda kufa hovyohovyo,la hasha.Walimaanisha kuwa kwenye maisha yao wamepata sababu zenye nguvu na msingi zaidi kuliko kuishi ili kula, kunywa, kununua gari, kuoaau kuolewa na kuwa na watoto. Wanamaanisha kuwa kama unataka kuwa mtu unayeleta tofauti katika kizazi chako ni lazima uwe mtu uliye tayari kujitoa kwa ajili ya wengine.Siku moja mwaka 2002 wakati nasoma biblia nilikutana na ujumbe wa Mwanzo 45:5,”
..Yusufu akawaambia kaka zake,Ingawa ninyi mliniuza ila Mungu alikusudia Kunitanguliza ili niwasaidie(To save your life)”Nikasikia ujumbe ndani yangu-“Nawe umetumwa ili uwasaidie wengine”.Kuanzia hapo nilianza kujifunza mambo mengi sana na kujaribu kufanya kila nililoweza kwa ajili ya kuchangia mafanikio ya wengine.
Mabadiliko katika nchi yoyote yanaletwa pale kunapokuwepo na watu walio tayari kuishi maisha ya kujito, najua unasoma ujumbe huu kwa sababu wewe ni mmoja wao.Kumbuka kile Mama Theresa Alichosema-“Hakuna anayeweza kuwasaidia watu wote,lakini kila mtu anaweza kumsaidia angalau mtu mmoja”
Watu wanaoleta mabadiliko katika kizazi chao ni watu ambao wanaamini kuwa wanao wajibu mkubwa kwa jamii yao bila kujali nafasi waliyonayo kwa sasa.Angalia kile ambacho unatamani kibadilike na chukua hatua ya kubadilisha.
Safari ya kuchangia mabadiliko katika jamii na nchi yako yanahitaji uvumilivu sana,usikubali kukata tamaa kwa sababu ulifanya kitu hakikuwa na matokeo.Katika nchi nyingi watu wanaosimamia haki na mabadiliko ya dhati huchukiwa na watu wabaya wako tayari kuwaondoa duniani.
Tunahitaji kizazi kipya cha watu ambao si wale walio tayari kumwaga damu za wengine ili wao wabakie katika nafasi bali wale walio tayari kutoa uhai wao ili kuokoa uhai wa wengine.Wako wapi akina Mandela wa leo ambao hawakusukumwa na cheo bali walisukumwa na ukombozi wa mtu mweusi.
Wako wapi akina Nyerere wa leo ambao hawakusukumwa na kutafuta umaarufu na utajiri kupitia nafasi zao bali walisukumwa na uzalendo na upendo kwa nchi yao,ambaye hadi anakaribia kukata roho bado anasema-“Najua Watanzania watanililia,lakini nitawaombea kwa Mungu”
Ile sauti najua haikuwa ya peke yangu,najua nawe unaisikia ndani yako,najua kipo kizazi kipya kinachoamini katika kujitoa kwa ajili ya jamii na nchi yao sio kwa ajili ya faida yao wenyewe bali kwa ajili ya faida ya wengine na kizazi kijacho.
Patrice Lumumba ambaye hata mifupa yake iliyeyushwa kwa tindikali ili kufuta ushahidi ,sauti yake bado inalia kutoka katika misitu ya kongo kwenda kila nchi ya bara la Afrika-Inalia na kuita "Wako wapi Vijana wa kizazi cha leo walio tayari kujitoa kwa nchi yao?” Nawaza kwa Sauti
Shukran: Joel Arthur Nanauka
Habari Zingine
Mjulishe Mwenzako
0 MAOINI :