Huyu ndio Mkenya aliyepambana na Mohammad Ali alipozuru Kenya mwaka 1980

Posted in
No comments
Tuesday, June 7, 2016 By danielmjema.blogspot.com


Bado dunia na mashabiki wa mchezo wa Boxing wapo katika maombolezo ya msiba wa bondia mahiri aliyewahi kushinda mikanda mbalimbali ya Boxing Duniani Muhammad Ali.

Katika mitaa ya pembezoni ya Jiji la Nairobi, eneo la Baba Dogo, kilomita chache kutoka uliko uwanja wa kimataifa wa Moi, Kasarani, katika kajumba kadogo kuukuu, anaishi Mzee mmoja anayefahamika kwa jina la Mohammed Abdalla Kent, maarufu kama Mohammed Ali wa Kenya.

Unaweza ujiulize inakuaje mzee huyu akapewa jina la Bondia huyo maarufu ulimwenguni liyefariki Dunia Siku ya Jumamosi, Juni 4, mwaka huu, lakini jibu la kwamba kati ya Mabondia wote maarufu unaowafahamu humu nchini na ukanda zima la Afrika mashariki, ni Kent pekee ndiye aliyepata fursa ya kuingia ulingoni na Shujaa huyo, alipozuru Kenya, mwaka 1980.

Kent ambaye licha ya umri kwenda sana, bado hanaonekana kuwa na nguvu, mwili uliojengeka anasimulia mengi yaliyotokea mpaka akafikia kuingia ulingoni na Bigwa huyo wa zamani mara tatu wa mkanda wa WBO, wakati ambapo kulikuwa na mabondia wakubwa nchini ambao walikuwa na nafasi kubwa ya kufanya hivyo.



Ilikuwa ni Ijumaa ya Februari 6, mwaka 1980, katika kituo cha Starehe, Starehe Boys Centre ambapo Kent akiwa bado ni bondia wa kawaida anayechipukia alipata fursa ya kukutana na Ali kabla ya kukabiliana nae ulingoni.

“Nilikuwa nimereja nchini nikitokea katika mashindano ya Olimpiki ya mwaka 1980, yaliyofanyika Ujerumani, sikuwa nafahamu kama Mohammed Ali yuko nchini, sikujua ningekutana nae, nilipojua yupo nchini, niliungana na wenzangu kwenda Starehe kumuona uso kwa uso bila kujua kama ningepanda naye Ulingoni,” anasema Kent na kuendelea.

“Mwenyekiti wa ngumi za ridhaa wakati huo, Marsden Madoka, aliponiona miongoni mwa watu waliofika kumuona bingwa huyu, alinifuata na kuniambia tafadhali, tunataka ufanye ‘Sparring’ na Ali, nilimkatalia maana kulikuwa na mabingwa kama James Omondi kwanini iwe mimi?” anasema Kent


Anasema alikubali kupanda ulingoni baada ya Madoka kusisitiza kuwa yeye ndiye anayeweza kufanya kile walichokidhamiria ambacho ni kumpa changamoto mgeni wao (Ali), pia aliniambia wengine wote walikuwa wamekataa, ilibidi nikubali shingo ukizingatia (Madoka) alikuwa ni bosi wangu.

 “Nilikubali huku nikujiambia kimya kimya kwamba nikiona maji yanazidi unga, nanyanyua mikono, maana katika mchezo wa ngumi hakuna mechi ya majaribio, mpambano ni mpambano, ngumi huwa hazichagui muda wa kuingia, Nilipewa Glovu na bondi mmoja anaitwa Athuman Ali,”

Mara tu baada ya pambano hilo la kirafiki kuanza, Kent aliwashangaza watu baada ya kumtwanga Ali katika raundi zote nne za mwanzo, lakini ‘The Greatest’ aliweza kujikusanya na kumtwanga kwa ‘knockout’.

“Nilianza kumshambulia nikilenga maeneo ya tumboni, kwa sababu nilijua nikilenga eneo la juu la mwili wake, ningekuwa katika hatari ya kujiingiza mkenge na kujikuta nikiambulia ngumi zake kali, langu liko fiti ‘I am fit, my belly is fit’, anasimulia Kent.

“Wakati wa mapumziko ya raundi ya pili, Madoka aliniimiza niwe nalenga kila mahali ambayo nahisi itamnyong’onyeza katika mwili wake, tuliporudi kwa ajili ya raundi ya tatu, nilimtwanga katika eneo la kidevu na kufanikiwa kumuangusha, nilifurahi sana”

Baada ya kumuangusha Ali, Kent anasema alikuwa anajiandaa kwa ushindi lakini furaha yake iliyeyuka ghafla.  “Nilivyoamuangusha, Mwamuzi alihesabu hadi saba, nikawa najua huyu haamki tena lakini ghafla jamaa alinyanyuka, alianza kunishambulia mfululizo, alinitwanga ngumi zito la kushoto  shingoni, na kunipeleka chini, nakumbuka nilipiga kelele nikisema, ‘Mohammad unaniumiza’ akanijibu ‘jilinde’

Nguvu na kasi

Kent anaendelea kukumbuka pambano hili la historia kati yake na marehemu Mohammad Ali, ambapo namwagia sifa Shujaa kwamba alikuwa na nguvu sana na kwamba aina yake ya upambanaji pia ulikuwa ni tofauti kwani alikuwa na uwezo wa kurusha ngumi nyingi za haraka haraka bila kuchoka.



“Alinirushia ngumi sita za haraka haraka kwa kutumia mkono wa kushoto, na uzito wa hizo ngumi ungedhani ni mkono wa kulia, ilikuwa ni kama burudani fulani hivi, baada ya kumaliza pambano hilo, nakumbuka Ali aliniambia nina uwezo wa kupigana nchini Marekani.”

Maisha ya Kent

Mohammad Abdalla Kent ambaye jina lake halisi ni Simon Kent, alizaliwa Septemba 20 1953, lakini kama ilivyokuwa kwa Mohammad Ali, ambaye jina lake halis lilikuwa ni Cassius Clay kabla ya kubadili dini na kuwa Muislamu, Kent naye alibadili dini na kuwa muislamu na ndio mwanzo wa jina Mohammad Abdalla Kent.

“Nilienda Marekani, nikapata fursa ya kusoma tafsiri ya Quran, nilishawishika kubadili dini na kuwa muislamu. Jina la Kent nimeliasili kutoka kwa Mama yangu lakini jina la Abdalla nililiasili kutoka kwa Muislamu mmoja ambaye ndiye aliyeniongoza wakati naingia katika uislamu, na jina Mohammad nilichukua la Lejendari, Mohammad Ali.”

Anasema Mama yake alimkataza kuingia katika Ndondi, lakini baadae alikubaliana nae baada ya kumaliza shule ya msingi, mwaka 1966, katika shule ya msingi ya Jericho.

Habari Zingine

0 MAOINI :

Fadhili Athumani



EastAfrica Swahili Blogger, Journalist at Mwanaspoti Kenya, Nairobi Kenya, Call: +254705246475, whatsapp:+255654724337, Email: fadhiliathumani85@gmail.com

Proudly Powered by EAMG .