POLISI KILIMANJARO YANASA WATOTO 11 WAKIWA WAMEFICHWA NDANI YA CHUMBA HUKO LYAMUNGO

No comments
Thursday, March 12, 2015 By danielmjema.blogspot.com

Na Happiness Tesha, Kilimanjaro.

SIKU chache baada ya kugundulika nyumba iliyohifadhi watoto 18 katika eneo la Pasua mjini Moshi mapya yameibuka baada ya  uwepo wa watoto wengine 11, wenye umri wa miaka 14 hadi 17,  katika nyumba nyingine  huko Lyamungo, wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro.

Kamanda wa polisi mkoani hapa  Geofrey Kamwela, amethibitisha kuwepo kwa kituo hicho kinachotambulika kwa jina la Umm  Sukhail,  kinachosimamiwa na mtu aliyefahamika kwa jina la Abubakar  Sekievu(64), mbondei, mwalimu mstaafu wa shule za  msingi, ambaye kwasasa anaishi maeneo ya Kibosho Mweka.

Alisema watoto hao  ambao  ni wajinsia ya kike  ambao wanatoka mikoa mbalimbali ikiwepo Dodoma, Singida, Tanga, Tabora, Mbeya na Kilimanjaro, ambapo watoto watatu katika hao ni wa mmiliki wa hicho kituo.

Kamanda akizungumzia mazingira ya kituo hicho na kilichokuwepo pasua,  alisema walikuta watoto hao wakifundishwa masomo ya dini ya kiislam na kushona nguo ambapo walikuta vifaa vya kushonea mahali hapo.

Alisema kituo hicho hakipo kisheria kwani hakijasajiliwa na wala hakitambuliki rasmi, ambapo  mazingira ya eneo hilo sio rafiki ya kuweza kuishi na kujifunza  kwa watoto hao kwani ni mazingira magumu.

Kamanda alisema jeshi la polisi linamshikilia mmiliki wa kituo hicho kwaajili ya upelelezi zaidi ili kujua kama kuna uhusiano wowote na kituo kilichogundulika pasua na kujua watoto hao baada ya kumaliza hayo mafunzo wanayowapa wanapelekwa wapi na je wanapata vyeti au laa.

Alisema jeshi la polisi linatoa wito kwa wananchi kutoa taarifa haraka endapo watabaini uwepo wa shule ambazo zinatoa masomo ya kidini bila utaratibu  wowote na ambavyo havijasajiliwa.

Katika tukio la watoto 18 waliokuwa wamefungiwa ndani eneo la Pasua
mkoani hapa,Jeshi la Polisi limeeleza kuwa tayari watoto hao wamekwishachukuliwa na wazazi wao huku wakiacha maswali juu ya kuachishwa kwao masomo na kuwepo katika kituo hicho kinachodaiwa
kufundisha masomo ya dini.


Kamanda Kamwela alisema kuwa idadi kubwa ya watoto hao umri wao unaonesha kuwa wangetakiwa kuwepo shuleni ambao wengi ni elimu ya msingi, lakini walikuwa kwenye kituo hicho bila kuwepo kwa taarifa za kuacha masomo au uhamisho.

Hata hivyo katika kuwahoji baadhi ya wazazi waliojitokeza kuwachukua watoto wao walikuwa na majibu tofauti,ikiwemo kuwa wamewapeleka kupewa elimu,huku wengine wakiwa wamepelekwa bila ridhaa ya wazazi.

“Licha ya kwamba wazazi wamekwishajitokeza kuwachukua watoto hao bado tunaendelea na uchunguzi, kujua walikuwaje wakawepo kwenye kituo hicho ambacho kinafudisha dini pekee,na pia walikuwa wakiishi katika mazingira magumu”Alisema Kamwela.

Mwisho.                                

Habari Zingine

0 MAOINI :

Fadhili Athumani



EastAfrica Swahili Blogger, Journalist at Mwanaspoti Kenya, Nairobi Kenya, Call: +254705246475, whatsapp:+255654724337, Email: fadhiliathumani85@gmail.com

Proudly Powered by EAMG .