HUYU NDIYE MWALIMU NA WENZAKE WALIOKAMATWA NA MIFUPA YA ALBINO KAHAMA
Posted in
Habari na Jicho Pevu la Kijiwe
No comments
Saturday, May 23, 2015
By
danielmjema.blogspot.com
Mwalimu Bahati Kilungu Maziku.
Waganga wa jadi Elizabeth au Shija Makandi Sweya (kushoto) na Regina au Tatu Kashinje Nhende.
Bilia Masanja Mhalala
Mganga wa jadi Abubakar Ally Magazi
Muhoja John Shija. (Picha zote na Daniel Mbega)
Na Daniel Mbega, Kahama
WATU
sita, akiwemo Mwalimu wa Shule ya Msingi Katunguru iliyoko Kata ya
Wendele, Tarafa ya Msalala wilayani Kahama, wamekamatwa mjini hapa
wakiwa na vipande sita vya mifupa inayodhaniwa kuwa ya albino.
Taarifa
zilizopatikana mjini hapa zimeeleza kwamba, mwalimu huyo Bahati Kilungu
Maziku (56), Msukuma na mkazi wa Mtaa wa Mbulu katika Halmashauri ya
Mji wa Kahama, amekamatwa akiwa na watu watano, wakiwemo waganga wa jadi
watatu, katika harakati za kuuziana mifupa hiyo.
Wengine
waliokamatwa ni mganga wa jadi Bi. Elizabeth au Shija Makandi Sweya
(42), mkazi wa Busongwahala, Wilaya ya Nzega mkoani Tabora, Bilia
Masanja Mhalala (39), Msukuma, mkulima na mkazi wa Mogwa wilayani Nzega,
mke wa Biria ambaye ni mganga wa jadi Regina au Tatu Kashinje Nhende
(40), Msukuma na mkazi wa Mogwa.
Aidha,
watuhumiwa wengine waliokamatwa ni Muhoja John Shija (24), Mnyamwezi na
mkazi wa Isagenhe wilayani Nzega pamoja na mganga wa jadi na
mfanyabiashara Abubakar Ally Magazi (25), Mrundi na mkazi wa Nzega.
Taarifa
za uchunguzi wa awali zinaeleza kwamba, Mwalimu Bahati ndiye aliyesuka
mpango mzima akishirikiana na waganga wa jadi Bi. Shija Makandi ambaye
ndiye aliyeitafuta mifupa hiyo na Abubakar Magazi ambaye alikuwa
apelekewe ili ‘kuibetua’ (kuitengeneza) na kuzalisha fedha.
Watuhumiwa
watano wanadaiwa kwamba walifunga safari kutoka Nzega hadi Kahama kwa
Mwalimu Bahati, ambaye kwa mujibu wa maelezo ya awali, ndiye aliyejua ni
wapi ambako mifupa hiyo ingeuzwa, hivyo walikuwa wanakutana hapo kwa
ajili ya kugawana fedha.
Mifupa
hiyo inadawa kuhusishwa na tukio la kukatwa mkono wa kulia Bi. Muungu
Masaga Gedi (35) mwenye albinism, mkazi wa Kitongoji cha Mkuyuni, Kijiji
cha Buhekela, Kata ya Igoweko wilayani Igunga, ambalo lilitokea Mei 16,
2014 na kufunguliwa Jalada Namba IGU/IR/1070/2014.
Katika
tukio hilo, mume wa majeruhi huyo, Mapambo Mashili, aliuawa kwa kukatwa
mapanga na watu wasiofahamika wakati akipambana na watu hao wasimdhuru
mkewe.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, SACP Justus Kamugisha, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo Mei 21, 2015 na kwamba watu
hao walikamatwa saa 7:00 mchana katika nyumba moja ya kulala wageni
inayofahamika kwa jina la Maji Hoteli iliyopo Phantom, Kata ya Nyasubi mjini Kahama baada ya Polisi kuweka mtego kufuatia taarifa za wasamaria wema.
Taarifa
ya Kamanda Kamugisha imesema kwamba, mnamo Mei 19, asubuhi, mkuu wa
upelelezi wa Wilaya ya Nzega alipata taarifa kuwa kuna mtu anauza viungo
vya albino, ndipo walipoweka mtego. Hata hivyo, alisemai kuwa
walishindwa kuwakamata na baadaye mtu huyo alihamishia biashara hiyo
wilayani Kahama.
Hata
hivyo, jeshi la polisi bado linaendelea na msako dhidi ya watu wengine
wanaotajwa kwamba ndio walioitafuta mifupa hiyo, na kwa mujibu wa
taarifa za awali, ndio waliohusika na mauaji pamoja na kumjeruhi mama
huyo.
Habari Zingine
Mjulishe Mwenzako
0 MAOINI :