Kama ulipitwa; Hii hapa Hotuba ya Mh. Edward Lowassa (Mb) Kwenye Mkutano wa kutangaza NIA
Posted in
Siasa
No comments
Tuesday, June 2, 2015
By
danielmjema.blogspot.com
UTANGULIZI:
Ndugu
viongozi, wana-CCM na Watanzania wenzangu; Kwanza nianze kumshukuru
Mwenyezi Mungu aliyetufikisha hapa leo. Lakini pia niwashukuru nyote
mlioweza kufika hapa leo. Kipekee niwashukuru CCM wenzangu na
Watanzania kiujumla ambao wameendelea kuwa marafiki na kuniuunga mkono.
Hakika nimejawa na furaha.
Hii ni siku
muhimu kwangu na kwa nchi yetu. Leo nimeamua kuwaita ili kuwatangazia
rasmi azma yangu ya kuomba ridhaa ya chama chetu, Chama Cha Mapinduzi
(CCM), ili niteuliwe kukiwakilisha cha chetu kuwa Mgombea Urais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Naamini
historia itaihifadhi kama ni siku ambayo kwa mara ya pili katika maisha
yangu, nimejitokeza kuwania kuiongoza nchi yetu kupitia chama chetu.
Mara ya kwanza ilikuwa ni mwaka 1995 wakati wa uchaguzi wa kwanza wa
vyama vingi hapa nchini nilipojitokeza nikiwa pamoja na Rais Jakaya
Kikwete; Wakati
ule sote tulikuwa wanasiasa vijana.
Pamoja tulikwenda kuchukua fomu na
baadaye kwa pamoja tukazungumza na waandishi wa habari. Tulileta hamasa
kubwa pale tulipofanya jambo ambalo halikuzoeleka kwa Watanzania kwa
kutangaza kwamba yeyote atakayepita kati yetu, mwenzake ambaye
hatafanikiwa angemuunga mkono.
Ningeweza kujitokeza tena mwaka 2005 lakini nikaamua kwa dhati kumuunga mkono Rais Jakaya Kikwete.
Nikiwa
Mwenyekiti wa Kampeni niliwaongoza wenzangu kufanikisha ushindi mkubwa
wa mgombea wetu, na baadaye ushindi mkubwa wa asilimia 80 kwa Chama Cha
Mapinduzi kwenye uchaguzi mkuu wa 2005.
Nitaeleza
kwa nini nimeamua kujitokeza tena, na kwa nini naamini mimi ndiye mtu
sahihi wa kuiongoza nchi yetu wakati huu. Mpaka hapa itoshe tu kuwaeleza
ni kwa nini naamini leo ni siku muhimu. Ni siku muhimu kwa sababu nina
kiu ya kuona Watanzania wenzangu tunajiunga kuianza safari ya matumaini.
Ni siku
muhimu kwa nchi yetu pia, kwa sababu naamini inajibu wito wa mahitaji ya
sasa ya uongozi wa Taifa letu wa kumpata kiongozi imara atakayewaongoza
Watanzania kujenga taifa imara. Na hili nitalieleza kwa kina. Hii ndiyo
safari ya matumaini.
HALI YA NCHI NA MATARAJIO YA WATU:
Nchi yetu hivi sasa inapita katika kipindi kigumu, katika maeneo yote makuu ya kisiasa na kiuchumi.
Kisiasa,
tumeshuhudia kuongezeka kwa vuguvugu la mfumo wa vyama vingi, ambapo
ushindani kati ya vyama vya siasa unazidi kuwa mkali. Kwa bahati mbaya
ushindani huo umefikia hatua ya kuchukua sura ya kuonekana kama vile ni
mapambano ya watu binafsi badala ya kuwa mapambano ya sera na dira ya
kuongoza nchi.
Tunashuhudia
kuongezeka uhasama binafsi kati ya wanasiasa ndani ya chama kimoja
kimoja, na pia kati ya wanasiasa wa chama kimoja dhidi ya kingine.
Kadiri siku zinavyokwenda, hali inazidi kuzorota na ikiachiwa kuendelea
nchi yetu inaweza kujikuta mahali pabaya.
Kukua kwa
ushindani ni jambo jema linalokomaza na kurutubisha demokrasia yetu.
Tukiwa na ushindani wenye afya unaweza kuwa chachu ya kuleta mabadiliko
mema kwa wananchi, na kuchochea kasi ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii
katika nchi yetu.
Tunahitaji
uongozi imara katika kipindi hiki, ili kuondokana na siasa muflisi na
kujenga siasa mpya zinazoimarisha ushindani wenye tija unaojikita katika
kushindana katika kuwapatia huduma bora Watanzania. Hii ndiyo safari ya
matumaini
Kiuchumi,
tumeshuhudia ukuaji mzuri na kuongezeka kwa mapato ya ndani ya Serikali
na uimarishaji wa mfumo wa uwajibikaji na ulipaji kodi. Kwa upande
mwengine, Serikali ya Rais Benjamini Mkapa na Rais Jakaya Kikwete
zimefanya kazi kubwa katika uendelezaji wa sekta ya mafuta na gesi
asilia ambapo kiwango kikubwa cha gesi asilia kimegunduliwa.
Tanzania
sasa imekuwa ni miongoni mwa nchi zinazovutia uwekezaji mkubwa katika
sekta hiyo ambayo inatajwa kwamba inaweza kuja kubadilisha kabisa maisha
ya Watanzania. Hata hivyo, kipindi hiki kuelekea ujenzi wa uchumi wa
kisasa kimeshuhudia kuongezeka kwa hofu na wasiwasi miongoni mwa
wananchi kwamba hawatonufaika na ukuaji huu wa uchumi na ugunduzi wa
utajiri mkubwa wa gesi asilia.
Kwa upande
mwingine, vijana wanataka kuona ukuaji wa uchumi na ugunduzi wa utajiri
huo unakwenda sambamba na uzalishaji wa ajira zenye maana ili waweze
kukabiliana na changamoto za maisha yao.
Niliwahi
kusema kwamba tatizo la ukosefu wa ajira likiachiwa bila ya kutafutiwa
ufumbuzi ni bomu linalosubiri kulipuka. Vijana wasio na ajira hupoteza
matumaini na ni rahisi kughilibiwa kuingiza nchi katika machafuko.
Tunahitaji uongozi imara kuweza kuikabili hali hiyo na kuitafutia
suluhisho maridhawa. Hii ndiyo safari ya matumaini
WATANZANIA WANATAKA MABADILIKO:
Ndugu zangu,
mnaweza kujiuliza kwa nini nimeyaeleza yote hayo na yana mahusiano gani
na dhamira yangu ya kutangaza nia ya kutaka kuiongoza nchi yetu kupitia
CCM?
Watanzania
wanataka mabadiliko yatakayowawezesha kukabiliana na changamoto hizi na
kuwaongoza kujenga Taifa imara ambalo kila mwananchi wake anaishi akiwa
na uhakika wa usalama wa maisha yake, mali zake na mahitaji yake muhimu.
Papo hapo akijiridhisha kwamba leo yake ni bora kuliko jana yake, na
kesho yake itakuwa bora zaidi kuliko leo yake. Kwa maneno mengine,
Watanzania wanahitaji mabadiliko yatakayowapa uongozi imara, unaoweza
kuwaongoza kujenga taifa imara. Hii ndio Safari ya Matumaini.
Naamini
kwamba, hata katika kipindi hiki ambapo Watanzania wanataka mabadiliko,
na wanaendelea kuamini kwamba CCM ina uwezo wa kusimamia mabadiliko
hayo.
Lakini kama
alivyotuusia Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, mwaka 1995, wakati
wa uchaguzi mkuu wa kwanza chini ya mfumo wa vyama vingi hapa nchini,
Watanzania wasipoyapata mabadiliko hayo ndani ya CCM watayatafuta nje ya
CCM!
Sina shaka, CCM tunao uwezo wa kuwapa Watanzania mabadiliko wanayoyataka.
UONGOZI UNAOHITAJIKA KULETA MABADILIKO YANAYOTAKIWA:
Rais Jakaya
Kikwete amefanya kazi kubwa katika kipindi chake na kama ambavyo amekuwa
akisisitiza mara kwa mara katika hotuba zake za karibuni ni kwamba yeye
ametekeleza wajibu wake. Pia amesema anamwachia atakayemkabidhi uongozi
wa nchi yetu baada ya yeye kumaliza muda wake kuendeleza pale
atakapoachia.
Kwa maoni
yangu, ili kuifanya kazi hiyo na kuzikabili changamoto nilizozieleza,
nchi yetu inahitaji uongozi wenye sifa zifuatazo:
i) Uongozi wenye uthubutu, usioogopa kufanya maamuzi magumu;
ii) Uongozi thabiti, makini na usioyumba;
iii) Uongozi wenye ubunifu na wenye upeo mkubwa;
iv) Uongozi unaoamini katika mfumo shirikishi katika ujenzi wa Taifa;
v) Uongozi unaozingatia muda katika kutekeleza majukumu yake.
Naamini pia kwamba wananchi wanataka Rais ajaye wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania awe na sifa kuu zifuatazo:
1. Aweze kuwaunganisha Watanzania
2. Aweze
kubuni sera na kusimamia utekelezaji wa mikakati ya kuinua uchumi wa
Tanzania na kukuza pato la Mtanzania; ikiwemo kupunguza tofauti ya
kipato kati ya aliyekuwanacho na wasiokuwanacho;
3. Aweze kubuni sera na kusimamia utekelezaji wa mikakati ya kuzalisha ajira kwa vijana wetu;
4. Awe kuwa mfano wa kuchapa kazi na kuwajibika;
5. Aweze kusimamia vizuri ukusanyaji wa mapato na matumizi ya Serikali;
6. Aweze kutumia fursa yetu ya kijiografia kibiashara.
7. Aweze kusimamia matumizi ya raslimali zetu ili kuutokomeza umaskini wa Waatanzania
8. Aweze kutokomeza mianya ya rushwa kwa vitendo;
UONGOZI IMARA, TAIFA IMARA:
Naamini
kwamba uongozi wa juu wa nchi katika nafasi ya Urais si kazi ya
lelemama, na unahitaji utashi. Kabla hata ya kushawishiwa na wenzako, ni
lazima kwanza wewe mwenyewe uamini na uwaaminishe wenzio kwamba unao
uwezo wa kuwaongoza wananchi wenzako.
Kuamini kama
una uwezo na shauku, haina budi kwenda sambamba na uwezo wa kusimamia
yale unayoyaamini. Na kwangu haya mwili ni dhahiri. Nina ari, nina
shauku na nina uwezo, kama rekodi yangu inavyothibitisha.
Tunapomtafuta
Rais wa Jamhuri ya Muungano ni lazima tukumbuke kwamba tunamtafuta mtu
ambaye atakuwa pia ni Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama
katika nchi yetu. Na kwa Chama Cha Mapinduzi tunamtafuta mtu ambaye
atakuwa pia Mwenyekiti wa Chama chetu.
Naamini kwa
vigezo vyote, nina kila sifa ya kubeba dhamana hizo nzito. Katika mambo
ambayo najivunia, na sitoyasahau katika historia yangu ni kushiriki
kwangu kuilinda nchi yetu pale ilipohitajika. Nilishiriki kikamilifu
katika Vita vya Kagera nikiwa miongoni askari wa mstari wa mbele wa
mapambano.
Kutokana na
rekodi yangu inayoeleweka, naamini ninazo sifa za kuwaongoza Watanzania
wenzangu katika zama mpya za ujenzi wa Taifa la kisasa, lenye watu
wazalendo, walioshikamana na lenye uchumi imara unaomnufaisha kila
Mtanzania. Naamini ninao uwezo wa kuwapa Watanzania Uongozi imara kwa
ajili ya ujenzi wa Taifa Imara. Hii ndiyo safari ya matumaini
DIRA YANGU NA MATARAJIO YA WATANZANIA:
Najua kwamba
Ilani ya CCM ya mwaka 2015 imo katika hatua za mwisho za kukamilishwa
na itakapopata baraka za vikao vya Chama itakuwa ndiyo msingi wa
utendaji wa Serikali ya Awamu ya Tano itakayochaguliwa Oktoba mwaka huu.
Hata hivyo, naamini pia kwamba mgombea mwenyewe anayetaka ridhaa ya
Chama na ya Watanzania kuongoza nchi naye anapaswa kueleza dira yake.
Baada ya
kutafakari kwa kina changamoto tulizo nazo na matarajio na matumaini
waliyo nayo Watanzania, naamini kwamba Uongozi imara unaolenga kujenga
Taifa imara unapaswa kuwa na dira yenye malengo yafuatayo:
1.
Kuimarisha Muungano wetu kwa kuyashughulikia yanayotutenganisha na
kuyafanyia kazi ili yasivuruge yale yanayotuunganisha ambayo ni mengi
zaidi na makubwa zaidi.
2.
Kushughulikia matumizi mabaya ya siasa, za udini na ukabila na ubaguzi
wa aina yoyote, kwa kuimarisha siasa zilizoshiba uzalendo na zenye
kutuelekeza kwenye Utanzania wetu.
3. Kujenga uchumi imara na wa kisasa, na ambao ni shirikishi unaomnufaisha kila Mtanzania aliyeko mjini au kijijini.
4.
Kuondokana na sifa mbaya ya kuwa Taifa ombaomba. Kwa wingi wa rasilimali
tulizo nazo na neema ya ardhi, maziwa, mito na bahari, Tanzania tuna
kila sababu ya kuacha kuwa ‘bakuli la ombaomba’ na badala yake kuwa
‘mkoba wa neema’ katika Afrika. “We can transform our nation from being
the begging bowl to become the bread basket of Africa”.
5. Kujenga mfumo mpya wa elimu unaowatayarisha vijana wetu waweze kuajirika, kujiajiri na kushindana katika soko la ajira.
6.
Kuhakikisha ukuaji wa uchumi unenda sambamba kuhakikisha haki, usawa na
huduma za msingi za kila raia kama vile afya, maji safi nakadhalika.
Mambo haya
niliyoyaeleza hapa ndiyo yatakayokuwa msingi mkuu wa utendaji wa
Serikali nitakayoiongoza pale nitakapopewa ridhaa ya kubeba bendera ya
CCM katika nafasi ya Urais na pia nitakapopewa ridhaa ya kuliongoza
Taifa letu kupitia uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
RAMANI YA UONGOZI IMARA NINAOUAMINI (LEADERSHIP ROADMAP):
Kama
nilivyotangulia kusema, kazi ya kuongoza nchi si lelemama na hasa
unapoongozwa na dhamira ya dhati na msukumo wa ndani ya nafsi wa
kubadilisha maisha ya wananchi wenzako waliokuamini uwaongoze. Kwa
vyovyote vile, hiyo haiwezi kuwa kazi ya mtu mmoja. Ni kazi ya pamoja.
Hata hivyo, Nahodha, anayeongoza timu lazima awe na ramani
itakayomuongoza, yaani ‘Leadership Roadmap’.
Ndugu Watanzania, matatizo ya nchi yetu yanayotukabili sote tunayajua, kama nilivyoainisha hapo awali.
Serikali za
awamu zilizotangulia zimeyajadili na kujaribu kuyatafutia ufumbuzi. Mimi
pia nimekuwa sehemu ya jitihada hizi wakati wa utumishi wangu katika
chama na serikali huko nyuma.
Sasa mtauliza kama hii ndiyo hali halisi, ukiacha tu kuwa huu ni msimu mpya wa uchaguzi, kwa nini nagombea na ni kipi kipya?
Nimeamua
kugombea urais ili kupambana na umaskini. Ninapata hasira ninapoona
umaskini ambao ungeweza kuepukwa kutokana na raslimali nyingi
tulizonazo. Kinachohitajika hapa ni uongozi imara wa kutokomeza
umaskini.
Ndugu
Watanzania wenzangu, kama nilivyosema, Tanzania imepitisha sera na
sheria nyingi na mipango mizuri. Tunayo Dira ya Maendeleo ‘Vision 2025’
ninaamini sera na sheria zinajitosheleza. Umuhimu si wingi au upya wa
sera bali utayari na ubora wa utekelezaji wake.
Nia yangu ni
kuimarisha na kusimamia utekelezaji wa sera zilizo bora na kurekebisha
panapotakiwa ili kuchochea maendeleo ya watu yatakayosimamiwa na
serikali inayojali.
Kipya
ambacho uongozi wangu utaleta, ni mwanzo wa mchakamchaka wa maendeleo
katika misingi ya utawala bora, na utendaji utajengwa katika nguzo
zifuatazo:
1. Kurejea
kwenye Katiba katika kuainisha nia, dhamira na malengo yetu ya kujenga
jamii inayozingatia misingi ya demokrasia, udugu na amani.
Muhimu
katika hili ni kukemea na kuchukua hatua dhidi ya tabia mbaya,
zinazochochea mfarakano katika jamii kama vile matumizi mabaya ya siasa
za udini na ukabila.
Aidha moja
ya misingi muhimu ya Katiba ni Muungano wetu. Itakuwa dhamira yangu
kuimarisha misingi ya Muungano pamoja na udugu wa damu na historia ya
ushirikiano iliyojengwa na waasisi wetu, Baba wa Taifa Mwalimu Julius
Kambarage Nyerere na Hayati Sheikh Amri Abeid Karume na kuyaenzi
Mapinduzi matukufu ya Zanzibar.
2. Kujenga
fikra mpya za kurejesha kujiamini na kufufua azma ya kujitegemea kama
Taifa. Tuanze kwa kujipiga kifua kwa kujiamini kuwa tunaweza kujitegemea
na kuijenga Tanzania sisi wenyewe. Kujiamini na kujitegemea ndio uhuru
wa kweli.
3. Kujenga
uzalendo, uadilifu ikiwa ni pamoja na kuimarisha uwazi katika shughuli
zote za serikali na kupambana na rushwa. Tukumbuke kuwa hatuwezi kujenga
uchumi wa kisasa kama tutaruhusu rushwa ishamiri. Wawekezaji hawataleta
mitaji yao kwa wingi kama rushwa itaendelea kutawala katika huduma
serikali na wananchi hawawezi kupata huduma bora kama rushwa itaendelea
kutawala. Ni lazima tuipinge rushwa kwa vitendo sio maneno.
4. Kujenga
Serikali madhubuti, makini na yenye nidhamu inayoendeshwa kwa misingi ya
sheria, uwazi na uwajibikaji. Maendeleo ya watu hayawezekani bila
serikali kusimamia utekelezaji sera na miradi na kuleta ufanisi katika
kutoa huduma na kusimamia maendeleo. Tumekuwa wepesi wa kutunga sera
lakini wazito wa kuzitekeleza na kuzisimamia.
5. Kuleta
msukumo mpya wa ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi katika
ujenzi wa uchumi wa kisasa na unaojitegemea. Sekta binafsi ndiyo nyenzo
ya uchumi imara. Inazalisha mali, ajira na kuchangia kwa kiasi kikubwa
katika pato la taifa kwa kulipa kodi. Ili sekta hii itoe mchango
unaotakiwa katika maendeleo ni lazima ifanye kazi na serikali kwa
karibu. Tukumbuke, bila uchumi imara hakuna huduma bora!
6. Uwekezaji
katika huduma za jamii. Elimu na afya bora, michezo, mazingira, makazi
safi na maji salama ndiyo mihimili ya maendeleo ya watu. Hii inawezekana
tu iwapo serikali itakuwa na sera na utashi wa kuutambua uboreshaji wa
huduma za jamii kama ndiyo lengo kuu la maendeleo ya nchi. Napenda
kusisitiza kuwa, elimu ndiyo muhimili wa maendeleo, ndiyo mkombozi wa
kweli wa binadamu. Mimi ni mfano hai wa ukombozi wa elimu. Elimu ndiyo
imenivusha kutoka kijijini kwetu Ngarash na kunipa upeo wa kitaifa. Mama
akiwa na elimu atatambua umuhimu wa kumpeleka mwanae shule, anapata
lishe bora na chanjo stahili na kuwa anaishi katika mazingira safi.
Mkulima akipata elimu stahiki, atakuwa mkulima bora na kilimo chake
kitampa tija na kumletea maendeleo. Elimu ndilo silaha dhidi ya
umaskini, maradhi na ujinga.
7. Kujenga
uchumi shirikishi unaolenga kuondoa umaskini. Mkakati wa kuondoa
umaskini Tanzania lazima ujikite kwenye nguzo za ushiriki wa kila
Mtanzania katika uchumi wa taifa. Kwa misingi hii, tukiweza kupunguza
umaskini, tutaweza pia kupunguza ukubwa wa tofauti za kipato kati ya
walio nacho na wasionacho, ambazo tukiziacha ziendelee kukua kwa kiasi
cha sasa, zinawezakuhatarisha utulivu na amani katika jamii yetu. Uchumi
shirikishi ndio silaha dhidi ya umaskini.
8.
Kuimarisha ulinzi wa nchi na usalama wa raia na ujirani mwema. Itakuwa
nia yangu kuimarisha misingi iliyojengwa kulinda na kudumisha umoja na
amani nchini. Kadhalika, nitahakikisha kuwa usalama wa mipaka ya
Tanzania unaimarishwa kwa misingi ya ujirani mwema na kutanzua migogoro
na matatatizo yoyote na nchi jirani, kwa njia ya diplomasia na
mazungumzo.
HITIMISHO:
Hii ndiyo
misingi na dira ya uongozi wangu. Nachelea kusema kuwa haitakuwa kazi
rahisi. Lakini kwa ushirikiano wa kila mmoja na kufanya maamuzi magumu,
yote yanawezekana. Tumeona nchi nyingi zilizosimamiwa na utawala thabiti
wa serikali za kimaendeleo zikikabili na kupunguza umaskini katika
kizazi kimoja. Kama mataifa mengine yamefanikiwa, tena bila ya kuwa na
raslimali kama zetu, kwa nini sisi tushindwe?
Napenda kumalizia kwa kusisitiza yafuatayo:
1.Tutahakikisha
kuwa tunajenga uchumi imara ikiwa ni pamoja na kujenga viwanda na
kukuza utalii, kuboresha kilimo, uvuvi, mifugo na kuhakikisha kuwa
tunasarifisha mali ghafi badala ya kuuza mazao yetu nje.
2.Tutahakikisha
kuwa rasilimali za nchi ikiwa pamoja na gesi asilia zitatumika kwa
manufaa ya kila mwananchi kwa lengo la, kuondoa umasikini
3. Tutahakikisha kuwa tutakabiliana na rushwa kwa vitendo na si kwa maneno, na kuimarisha mshikamano wa taifa
4. Tutahakikisha tutaanza safari ya matumaini ya kuwapatia Wanzania elimu bora itakayoleta mapinduzi ya fikra.
5.Tutahakikisha tunaboresha maslahi ya walimu na ya wafanyakazi wengine wa sekta ya umma.
6.Tutaanza mchakato wa kuwapa watanzania matumaini mapya ya kujiwekea akiba na kunufaika na mifuko ya hifadhi ya kijamii
7. Tutahakikisha kuwa Watanzania wote wanapata huduma bora za afya, maji safi na salama
8.Tutahakikisha tunakabiliana na kutatua tatizo la ukosefu wa kazi kwa kubuni na kuongeza vyanzo vya ajira
9.
Tutahakikisha kuwa wafanya biashara wadogo wadogo na sekta isiyo rasmi,
kwa kama vile wamachinga, bodaboda na mama ntilie watawekewa utaratibu
bora zaidi wa kufanya na kuendeleza shughuli zao
10. Tumechoka kuwa kichwa cha mwendawzimu katika michezo na washiriki washindwa.
11.Tutatengeneza mazingira mazuri ya kuwezesha Watanzania waishio nje kuchangia kujenga na kukuza uchumi wa nchi yetu
12.
Tutaboresha miundo mbinu ili kukabiliana na adha ya msongamano katika
jiji la Dar Es Salaam, Arusha, Mwanza na Mbeya; ni lazima tulivalie
njuga jambo hili kuhakikisha linatatuliwa kwa haraka sana.
Ndugu Watanzania:-
Ni maono yangu kuwa siku si nyingi, nchi yetu itaanza safari yenye uelekeo wa matumaini na neema tele kwa wananchi.
Ni maono
yangu kuwa siku si nyingi sisi kama Watanzania, kwa umoja wetu
tutajivunia kuishi katika nchi tunayoipenda na inayoendeshwa kwa misingi
ya utawala bora, chini ya serikali ya kimaendeleo iliyojengwa kwenye
fikra mpya za uzalendo, uadilifu, utendaji na uwajibikaji.
Ni maono
yangu, siku si nyingi Watanzania watajikwamua kutoka katika janga la
umaskini na kwamba taifa letu litakuwa na uchumi imara na hatimaye
kujitegemea.
Mimi si mtu ninayeamini kuongoza taifa ambalo watu wake wanajivunia umaskini.
Huwezi ukawa
kiongozi ya nchi maskini, unayelenga kupunguza umaskini halafu ukawa
unashabikia umaskini na kuuona ni sifa ya taifa.
Tuna kila
sababu ya kufanya maamuzi magumu sasa ili kuwajengea Watanzania
matumaini mapya ya maendeleo. Tuanze pamoja mchakamchaka wa amendeleo
Watanzania
wenzangu, peke yangu sitaweza, lakini kwa maamuzi magumu na ushirikiano
wa wananchi wenzangu, inawezekana kuanza safari ya matumaini mapya.
Naomba
nihitimishe kwa kuwaomba wana CCM ikiwa ni pamoja na wagombea wenzangu,
waniunge mkono na tujumuike kwa pamoja katika safari hii ya matumaini. Safari tuianze leo, hatuna kesho nyingine.
Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Africa
Ahsanteni sana kwa kunisikiliza.
Picha na: Michuzi blog
Habari Zingine
Mjulishe Mwenzako
0 MAOINI :