KAMA ULIIKOSA; HII HAPA HOTUBA YA MWIGULU NCHEMBA
Posted in
Siasa
No comments
Tuesday, June 2, 2015
By
danielmjema.blogspot.com
Dodoma/Dar.
Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba ametangaza nia yake ya kugombea
urais kupitia CCM katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba akieleza jinsi
atakavyoivusha Tanzania kuwa nchi yenye uchumi wa kati utakaopatikana
kwa kutoa haki kwa watu wote.
Akitangaza
nia hiyo jana kwenye Ukumbi wa Mwalimu Nyerere katika Chuo cha Mipango
Dodoma, Nchemba alisema: “Ahadi yangu kubwa kwenu ni kwamba nitawavusha.
Nitawavusha wanaCCM wenzangu pamoja na Watanzania kwa ujumla… wakati ni
sasa tunataka Taifa letu lifike kuwa nchi yenye uchumi wa kati,”
alisema Nchemba na kuongeza:
“Ninachoomba
kutoka kwenu, mniamini na mniunge mkono katika hili… nitawavusha.
Lakini tukumbuke kwamba kila mmoja lazima atimize wajibu wake katika
utendaji kazi ili tufikie huko tunapotaka kufikia.”
Nchemba
aliyekuwa ameongozana na mkewe, Neema na watoto wake watatu, Isaack,
Grecious na Joshua pamoja na ndugu jamaa na marafiki, alisisitiza kuwa
ili kufikia malengo hayo, lazima nchi iwe na mfumo wa uwajibikaji
utakaowezesha kulinda rasilimali za Taifa na kuongeza Pato la Taifa.
Huku
akitumia kauli mbiu ya ‘Mabadiliko ni Matendo, Wakati ni Sasa’, ambayo
ataitumia katika safari yake ya kuelekea Ikulu, Nchemba aliyetumia
dakika 115, kuanzia saa 10.10 jioni hadi saa 11.25 jioni, alisema
atapambana na tabia za watu kufanya kazi kwa mazoea, rushwa, ufisadi na
kwamba Serikali ya Awamu ya Tano atakayoiongoza endapo atachaguliwa,
itakuwa ya uadilifu na uaminifu.
Alisema
iwapo atachaguliwa, ataifanya nchi kuwa ya kipato cha kati sambamba na
watu wake, kujenga Taifa linalojitegemea kibajeti na kuwajengea uwezo
wananchi kumiliki uchumi wao wenyewe.
Huku
akieleza jinsi atakavyomaliza kilio cha ukosefu wa ajira, wanafunzi,
wakulima, wafanyakazi, wafanyabiashara na watu wa kada mbalimbali
nchini, Nchemba alianza hotuba yake kwa kuwashukia baadhi ya watu wenye
dhana potofu juu ya mtu anayestahili kuwa rais wa nchi.
“Nimeamua
kutangazia nia hapa Dodoma kwa sababu ndipo makao makuu ya nchi na kama
nikiwa rais nitaapishiwa hapa. Pia sikutaka kutangazia nia nyumbani
Iramba ili kuondokana na umimi,” alisema na kushangiliwa na mamia ya
watu waliohudhuria mkutano huo.
Awajibu wanaomponda
“Uzoefu ni mazoea ya starehe. Mtu aliyekaa katika uongozi ni mtu aliyesahau shida za Watanzania.
Jambo la
kwanza na la msingi ni kuitambua ajenda ya Watanzania, Watanzania
watamuunga mkono kiongozi kwa kuitambua ajenda yake,” alisema.
Alisema
wakati akijitathimini kutangaza nia ya kugombea alikuwa akifahamu ajenda
ya Watanzania, huku akisisitiza kuwa umaskini hakuusoma katika vitabu,
bali amekulia katika maisha ya kimaskini.
“Ukizungumzia
ukosefu wa ajira na dawa hospitali hilo sijalisoma vitabuni,
ukizungumzia ajira kwa vijana na watu wote hilo jambo sijalisoma
vitabuni.”
Alisema
katika pitapita zake, amesikia habari za mtu anayefaa kuwa rais
zikihusishwa na umri na uzoefu, “Ujana na uzee haviwezi kuwa sifa ya
kuiongoza nchi. Kukaa serikalini muda mrefu haiwezi kuwa sifa ya kutosha
kuliongoza Taifa hili, unaweza ukakaa sana serikalini lakini
ukasababisha hasara kubwa.
Hata kuishi ni hivyohivyo, kinachoangaliwa si
kuishi miaka mingi, bali ni kipi ulichokifanya. Leo hii marehemu
(Edward) Sokoine hakumbukwi kwa sababu alikaa sana serikalini,
anakumbukwa kwa matendo yake kwa kipindi kifupi alichokaa serikalini.”
Huku
akishangiliwa alisema, “Kiongozi akipatikana kwa mazoea atafanya kazi
kwa mazoea. Vita ya kwanza tunayotaka kuikomesha katika nchi yetu ni
kufanya kazi wa mazoea. Tunahitaji mambo matatu; mabadiliko, mbinu za
kufanya mabadiliko na utayari wa kufanya mabadiliko.”
Kuhusu umri
alisema: “Wengine wanaongelea umri wamesahau kuwa Katiba inasema umri wa
kugombea ni miaka 40, hata vitabu vitukufu vimeandika kwamba umri wa
miaka 40 ni sahihi mtu kupewa utume na unabii, Mussa alipofikisha miaka
40 aliaminiwa kwenda kuwakomboa ndugu zake.”
Alisema hata Mwalimu Julius Nyerere alikuwa rais akiwa na miaka 40, tena akitoka kufundisha sekondari.
“Watu
wanataka kuwatoa Watanzania katika ajenda kwa kuzungumzia vitu vyepesi.
Eti wanasema ukimaliza kuwa rais wakati bado kijana utafanya nini.
Nifanye nini tena wakati nitakuwa nimeshamaliza kazi. Najipambanua kwa
ajenda yangu na wale watakaoniangalia wataangalia ajenda yangu,”
alisema.
Mipango yake
“Kwa miaka
50 tumekuwa tegemezi, sasa imetosha tunakwenda kujitegemea. Kujitegemea
ni kila mmoja kulipa kodi anayostahili,” alisema.
Alisema
wakati wa watu wachache kubeba mzigo wa kodi umefikia mwisho na kwamba
kila mtu anayestahili kulipa atailipa, awe mdogo au mkubwa.
“Tunakwenda
kuachana na utaratibu wa kukimbizana na wauza vitumbua kuwadai kodi.
Kujitegemea ni nidhamu ya matumizi na sasa tunakwenda kuziba mianya ya
rushwa,” alisema.
Alisema ili
uchumi umilikiwe na Watanzania wenyewe, lazima njia za kuwapatia watu
kipato ziboreshwe kwa sababu uchumi wa nchi unakua lakini wananchi bado
wanalia umaskini.
“Njia ya
kuwatoa hapo walipo ni kuongeza thamani ya mazao na kazi wanazozifanya
kwa sababu asilimia 70 ya Watanzania ni wakulima. Lazima wakulima
watafutiwe pembejeo na masoko. Tunatakiwa kutumia sekta binafsi ili kuwa
na viwanda vingi nchini,” alisema na kutoa mfano:
“Pamba ya
Tanzania inaweza kutumika kutengeneza sare za shule, za jeshi na viatu
kutoka katika viwanda vilivyopo nchini. Tuna wanafunzi zaidi ya milioni
nane na kila mwaka wanaandikishwa shule, kwa nini tulilie soko la nje
halafu sare zao tunanunua nje.”
Kuhusu
mafuta, Nchemba alisema kilimo cha alizeti kikiboreshwa kitazalisha
ajira nyingi na hilo linaweza kufanyika pia katika sukari, kahawa, chai
na korosho.
“Awamu ya tano, nchi itaingia katika uchumi wa viwanda na vijana watafanya kazi kwa kupokezana,” alisema.
Mwigulu
aligusia suala la Watanzania kutozwa kodi zisizokuwa na kichwa wala
miguu na zisizoendana na uzalishaji wa biashara husika, huku akitolea
mfano mama ntilie na wamachinga.
“Wakubwa
wakitaka kuwekeza wanapewa likizo ya miaka 10 ya kulipa kodi lakini
anayefungua saluni anatozwa kodi wakati akiwa anapaka rangi jengo hata
biashara hajaanza,” alisema na kushangiliwa.
Rushwa
Akizungumzia
rushwa alisema: “Rushwa hupofusha macho ya wenye akili na kurejesha
nyuma maendeleo na hupindisha ukweli na kuwanyima haki maskini.”
Alisema
awamu zote nne za Serikali zimejitahidi kupambana na rushwa, ila awamu
ya tano itakuja na njia tofauti kwamba atakayethibitika kupokea au kutoa
rushwa atachukuliwa hatua haraka ili iwe fundisho.
“Sasa hivi
mtu akikamatwa na rushwa kesi zimekuwa na mlolongo mrefu. Tutabadilisha
Sheria namba 11 ya Kupambana na Rushwa ili kuipa meno Takukuru iweze
kushughulika na suala hili na atakayebainika atafilisiwa, kufukuzwa kazi
na kufungwa,” alisema.
Alisisitiza:
“Habari ya mtu kula rushwa ya fedha nyingi na kuondolewa katika cheo
chake ni sawa na kumpa likizo, ni sawa na kumfanyia ‘send off’ kwa fedha
za walipakodi.”
Kufanya kazi kwa mazoea
Akizungumzia
suala la kufanya kazi kwa mazoea alisema: “Serikali ya awamu ya tano
itaondokana na ukiritimba unaoondoa ufanisi. Hakutakuwa na ucheleweshaji
wa kutoka kwa ajira kwa kisingizio cha kibali. Nchi hii ina upungufu wa
wafanyakazi kila wizara na taasisi.
Lazima
ufanyike utaratibu wa kujua idadi ya vijana wasio na kazi ili waweze
kupatiwa nafasi. Inakuwaje mtu anastaafu halafu unasema hakuna wa kuziba
pengo lake!”
Alisema
anazungumzia uchumi kwa sababu ameusomea na kusisitiza, “Kuna matatizo
kwenye mgawanyo wa keki ya Taifa. Leo hii watu wakipewa dhamana ya
kusimamia shirika la umma wanachokifanya ni kutafuna fedha za
walipakodi. Jambo hili haliwezekani maana kuna wajawazito wanalala
chini.”
“Haiwezekani
sungura akawa mdogo kwa baadhi ya Watanzania na sungura huyohuyo akawa
mkubwa kama tembo kwa baadhi ya Watanzania. Haiwezekani shirika la umma
wakalipana posho za juu huku watoto wa maskini wanakosa mikopo.
Nitakomesha rushwa kwa kuzingatia masilahi ya wafanyakazi,” alisema.
Alisema ni
wakati wa Tanzania kuwa nchi ya viwanda na katika kuthibitisha hilo,
hayatafanyika makosa tena katika uwekezaji wa gesi kwa kuweka wazi
mikataba na fedha zitakazotokana na mauzo ya gesi lazima zihifadhiwe
katika akaunti za benki za ndani ya nchi.
Kuhusu elimu na afya, alisema sasa umefikia mwisho wa wananchi kununua dawa.
“Kila
anayeugua anaambiwa akanunue dawa lakini kila mwaka mnasikia Serikali
inadaiwa fedha za dawa. Katika hili tutadhibiti kila kitu ikiwamo wale
wanaoiba dawa na tukimbaini tutamnyang’anya leseni yake na atakwenda
jela,” alisema.
Kuhusu elimu
alisema: “Miaka mitatu ijayo tutakuwa na wanafunzi wengi na tutahitaji
zaidi ya Sh700 bilioni kwa ajili ya mikopo, kazi iliyopo mbele yetu ni
kuweka chanzo maalumu kwa ajili ya elimu ya juu ili mtoto yoyote mwenye
sifa asikose nafasi ya kwenda chuo kikuu kwa sababu tu ya kukosa mkopo.”
Pia aligusia
suala la kuimarisha ulinzi na usalama na Muungano ambao alisisitiza
kuwa ni lazima ulindwe na kuifanya Zanzibar kuwa na uchumi wa viwanda.
Katika hotuba yake, Mwigulu alisema ili kumaliza migogoro ya wakulima na wafugaji ni lazima kugawa ardhi kwa kila upande.
Kura za wanaCCM
Katika
hotuba yake Nchemba aliwaangukia wanachama wa CCM akisisitiza kuwa
amejitathimini vya kutosha na anaweza kukiongoza vyema chama hicho na
Watanzania wote.
“Ahadi yangu
kubwa kwenu ni kwamba nitawavusha. Kabla ya kufika kwa Watanzania
nitaomba ridhaa ya wanaCCM. Ninakijua chama hiki na ahadi yangu kwenu
nitawaunganisha wanaCCM na Watanzania wengine,” alisema.
“Tunakwenda
kukomesha kufanya kazi kwa mazoea na kusimamia rasilimali na kuweka
usawa, haya ndiyo tunasema ni mabadiliko kwa vitendo na wakati wa
kufanya hayo ni sasa. Taasisi zote za usimamizi nafasi zake zitapatikana
kwa ushindani,” alisema.
“Anayeanzisha
kibanda cha kibiashara lazima aandaliwe mazingira ya biashara yake.
Tunawahamisha wamachinga kwa kigezo cha kusafisha jiji utadhani wao ni
uchafu. Ukiwaondoa wakati walikuwa wakifanya kazi halali watarudi na
kufanya kazi zisizo halali,” alisema.
Alisema
anaomba ridhaa kwa wanaCCM ili akafanye kazi mapinduzi katika Taifa na
kuleta haki, heshima na upendo katika eneo lililotawala na chuki.
“Naomba
mambo matatu, kwanza mniamini, mniunge mkono na jambo la tatu
nitawavusha. Kwenye vita ya umaskini mimi ni mtu sahihi, wakati sahihi
na muda sahihi ni sasa,” alisema.
Ajibu maswali
Alipoulizwa
kuhusu hotuba yake ya kama haimhatarishii mbio zake za kuelekea Ikulu,
Nchemba alisema hana shaka na chama chake wala Watanzania na ndiyo maana
amesema atawavusha.
Kuhusu
atakavyoshughulikia rushwa kubwa kama za EPA, Meremeta na Escrow ambazo
watuhumiwa wake wameonekana wakitanua na fedha hizo, alisema sifa moja
ya mtu anayeweza kupambana na rushwa ni yeye kutokuwa mla rushwa.
Alisema
iwapo atapata ridhaa ya Watanzania, rushwa litakuwa ni janga na hivyo
litashughulikiwa kama tatizo maalumu... “Adhabu kali itatolewa ili mtu
asirudie tena kufanya hivyo.”
Alisema siyo
rushwa kubwa tu, bali nyingine zinazotokana na ununuzi wa umma ambao
watu wamekuwa wakipandisha juu bei ya bidhaa... “Hatutakuwa na uvumilivu
katika mazingira haya.”
Ilivyokuwa
Kuanzia saa
7.00 lango la ukumbi wa Mwalimu Nyerere katika Chuo cha Mipango na
Maendeleo ulikuwa wazi na idadi kubwa ya watu walianza kuingia wengi
wakiwa vijana kutoka mikoa ya Dodoma na Singida huku kukiwa na idadi
kubwa ya viongozi wa dini.
Wabunge
waliohudhuria ni Ally Keissy, Omary Badwel, Modestus Kilufi, Martha
Mlata, Asumpta Mshama na baadhi ya wabunge kutoka Zanzibar.
Mbali na
madiwani, makatibu na wenyeviti wa CCM kata na mitaa kwa Manispaa ya
Dodoma, Katibu wa CCM Mkoa Albert Mgumba na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya
CCM, Anton Kanyama.
Wengi wa vijana waliovaa fulana za rangi za Bendera ya Taifa huku wengi wakivaa skafu kama anavyovaa wakati wote Nchemba.
Baba mzazi
wa Mwigulu, Mzee Madelu Nchemba na mama yake, Asha waliongoza
wanafamilia ya Naibu Waziri huyo kutoka Kijiji cha Makunda Wilaya ya
Iramba mkoani Singida.
Nje ya
ukumbi, mabango yaliyojaa picha zake yalipambwa zikiwa na maandishi,
“Mabadiliko ni kwa vitendo, wakati ni sasa,” ambayo wengi walikuwa
wakipiga picha hapo. Mengine ni kupanga ni kuchagua na kutenda ni kwa
vitendo, wakati ni sasa.
Mabango
yaliyobebwa na vijana yalikuwa na ujumbe mbalimbali ukisomeka, Mwigulu
mkombozi wa Watanzania 2015, Mwigulu ni Sokoine aliye hai 2015 njia ni
nyeupe.
Habari na Fidelis Butahe, Sharon Sauwa, Suzan Mwillo,
Habel Chidawal na Raymond Kaminyoge
Picha na Edwin Mjwahuzi
Chanzo : Mwananchi
Habari Zingine
Mjulishe Mwenzako
0 MAOINI :