KAMA ULIMISI HII NDIO HOTUBA YA WASSIRA

Posted in
No comments
Tuesday, June 2, 2015 By danielmjema.blogspot.com


Mwanza/Dar. 
 
Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira ametangaza nia ya kuwania urais akisema iwapo CCM itampa ridhaa ya kupeperusha bendera yake, atahakikisha utendaji wa Serikali yake unakuwa wa kitaasisi.

Alitangaza nia hiyo katika Ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Mwanza jana Wasira alisema: “Baada ya kutafakari kwa makini nimeona uamuzi wa kugombea nafasi hii ya juu kabisa kwa nchi yetu ni sahihi na wakati muafaka, kwa kuwa nina nia ya kupeleka nchi hii katika ngazi ya juu kabisa ya kisiasa, kiuchumi na kijamii.” 

Katika hotuba yake iliyorushwa moja kwa moja na vituo vya televisheni vya ITV na Star TV, Wasira alisema: “Leo nakuja hapa Mwanza kuvunja ukimya na kumaliza minong’ono kwa kutangaza rasmi kwamba nimekata shauri ya kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.”

Wasira aliyekuwa ameongozana na mkewe na baadhi ya viongozi wa CCM, alisema angependa kuwaeleza Watanzania ni kwa nini amechukua uamuzi huo kwa kuwa jambo hilo si dogo.

 “Kwanza ni haki yangu. Raia wote wana haki ya kugombea, ni haki ya kikatiba. Lakini ninayo sababu nyingine ambayo ni kubwa zaidi, naifahamu vizuri Tanzania kwa muda mrefu tangu miaka ya 1970 nimeshirikishwa katika uongozi wa Taifa hili nikiwa na miaka 25,” alisema Wasira akibebwa na historia ya utendaji ya muda mrefu.

Wasira alitamba kuwa iwapo atateuliwa na CCM na kushinda urais, Serikali yake itasimamia uadilifu na kupambana na rushwa na amedhamiria kupandisha viwango vya maendeleo. Aliwaonya Watanzania kutothubutu kuukabidhi urais kwa mla rushwa, kwani kuna siku atauza Ikulu.

“Ili kukabiliana na changamoto hizi kubwa, itakuwa lazima kwa chama chetu kumteua mgombea ambaye hana historia ya kuhusishwa na ufisadi, iwe kwa kutuhumiwa tu au kuhusika kweli. Mgombea anayejua historia ya nchi yetu, pale ilipo na kule inakopaswa kuelekea.”

Akimnukuu Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere mara kwa mara, Wasira alisema kiongozi huyo aliwahi kusema kuwa rais wa Tanzania ni lazima achukie rushwa na anatakiwa aonekane kwa vitendo akiichukia... “Siku hizi kila kiongozi anakemea rushwa kama fasheni hata wala rushwa wanaikemea kwa sababu bila kufanya hivyo wanaona mambo yao hayatawanyookea.”

Kauli hiyo ya Wasira iliwafanya wafuasi wa chama hicho kusimama na kumshangilia huku wakiimba ‘Wasira sema usiogope.’

Alisema: “Mwalimu Nyerere aliwahi kuniuliza ninataka nini kati ya utajiri na kuongoza watu, alisema nikitaka utajiri nichague kuwa mfanyabiashara kwani nitanunua kwa bei rahisi na kuuza aghali.”

Alisema Nyerere alimweleza kuwa hawezi kuwa tajiri kwa kazi ya kutumikia watu kwa mshahara na kwamba mfanyabiashara ndiye anaweza kutajirika.

“Kwa hiyo nimewatumikia Watanzania katika nafasi mbalimbali tangu nikiwa na umri wa miaka 25 lakini sijawahi kuhusishwa na kashfa za rushwa, nyie ni mashahidi sijawahi kuhusishwa na kashfa za Epa wala Tegeta Escrow,” alisema.

Alisema hahusishwi na masuala ya rushwa kwa sababu alichagua kuwa mtumishi wa watu na kwamba hawezi kutajirika kwa kazi hiyo na ndiyo maana hana tamaa.

Alisema ukiona mtumishi wa watu anatajirika, basi ufahamu kwamba ni mla rushwa kwa sababu mshahara  hauwezi kumtajirisha.

Wasira aliyewahi kuzuiwa kuwania ubunge na Mahakama ya Rufani kwa tuhuma za kutoa rushwa, alisema akiwa rais ataliweka tatizo la rushwa kuwa katika mjadala wa kitaifa ili kupata mbinu mbadala za kumaliza tatizo hilo.

“Mnaweza mkanipima hapa kuhusu rushwa siyo kwamba siongozi wizara zenye mamlaka, hapana! Ningeweza kuuza mbolea yenu. Hatutaki mtu kuzungumzia rushwa kama fasheni, tunataka tukuone usoni na moyoni kuwa unachukia rushwa,” alisema.

Mamlaka za mikoa, wilaya
Alisema Serikali yake itahakikisha tawala za mikoa na wilaya zinapewa kipaumbele katika ukuaji wa mabadiliko kwenye maeneo yao.

“Kipaumbele kitawekwa kwenye ushiriki wa jamii katika maendeleo, kitawekwa kuhamasisha ushiriki, umiliki na usimamizi wa maendeleo ya mahali kwa kuzingatia mageuzi yao. Nitatekeleza dhana ya ‘korido za maendeleo’ ili wakulima wanufaike na unafuu wa gharama kwa sababu ya kufanana kwa kanda za mazao ya kilimo ambazo mara nyingi huvuka mipaka ya kiutawala ya mikoa.”

Alisema uchumi wa mahali utafanya mageuzi yake kuingizwa kwenye ajenda ya maendeleo wakati uanzishwaji viwanda kupitia usindikaji na kuongeza thamani, utahamasishwa na vichocheo vitakavyotumia fursa ya ukuaji na mageuzi kwa wote.

Miundombinu
Waziri huyo alisema Tanzania inahitaji miundombinu mingi kuanzia vinu vya kufulia umeme hadi mifumo ya usambazaji majisafi, viwanja vya ndege, bandari, mitandao ya barabara, reli na mawasiliano ya simu.

“Utawala wangu utaweka kipaumbele cha hali ya juu ili kuhakikisha uwapo wa miundombinu ya uhakika na gharama nafuu kwa ajili ya wazalishaji na walaji kuendana na ukuaji wa juu unaomfaidisha kila mmoja,” alisema.

Wasira, ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya kuandaa Ilani ya CCM 2015-2020, alisema serikali yake itaweka kipaumbele katika maeneo matatu makuu ili kupata matokeo kwa miaka mitano, aliyataja kuwa ni kuongeza uzalishaji umeme hadi megawati 7,000 ifikapo mwaka 2025.
Eneo jingine alisema ni kujenga njia za reli kuunganisha bandari kandokando ya bahari, kwenye maziwa na vituo vya mkakati vya kuvutia mipaka ya nchi na maeneo yote muhimu ya uzalishaji. Pia, ili kuhakikisha mawasiliano yenye kasi ya hali ya juu ya intaneti yanafika katika majiji, miji na vijiji vyote.

Afya
Wasira alisema Serikali yake itahakikisha huduma za bima ya afya zinapatikana kwa wote.

“Uwekezaji wetu wote katika elimu, utengenezaji wa nafasi mpya za ajira, miundombinu na utawala bora vitakuwa na mafanikio kidogo kama hatutazingatia afya za raia wetu. Utawala wangu utaweka dhamira ya kujenga huduma bora za afya itakayowahudumia watu wote. Bima ya afya, hasa ya jamii, itapewa kipaumbele kuimarisha upatikanaji wa huduma bora za afya.”

Alisema licha ya kuwapo mafanikio na kuongeza idadi ya wataalamu wa afya na hospitali nchini kwa miaka 50 iliyopita, huduma zake hazilingani na mahitaji kwani watu wengi hawawezi kupata tiba kwa sababu ya umaskini.

“Wale wanaomudu gharama za matibabu wanakimbilia nje kuyapata. Utaratibu huu unaligharimu Taifa fedha za kigeni… hivi sasa deni linazidi kulimbikizwa kwenye hospitali hizo kama India, watu wetu wengi wanaishi na magonjwa yanayotibika lakini taratibu yanawadhoofisha kisha kuwaua,” alisema Wasira.

Elimu
Iwapo atapitishwa na CCM na hatimaye kuchaguliwa kuwa rais, Wasira alisema utawala wake utaweka dhamira ya kuunda upya elimu ya Tanzania ili kuandaa rasilimali watu yenye weledi wa kutosha yenye kufaa kwa sekta ya umma na binafsi.

“Tutaweka mkazo wa kuleta ubora wa elimu ngazi zote kwa kuandaa mitaala (mitalaa) kamilifu kwa ajili ya elimu bora, hasa kwa kuwekeza katika walimu wa kutosha na walioiva vyema na mazingira ya kazi ili yaendane na idadi kubwa ya uandikishaji,” alisema.

Uchumi
Wasira alisema dira ya serikali ya awamu ya tano ni kujenga uchumi imara wenye kuleta ushindani na mkazo mkubwa kwenye serikali yake itakuwa kuleta maendeleo yanayomjumuisha kila mmoja.

Alisema anataka kuhakikisha kila Mtanzania anapata nafasi ya ajira yenye hadhi ili aweze kushiriki kwa namna yenye tija katika michakato ya ukuzaji wa uchumi.

“Serikali yangu itajenga katika misingi iliyowekwa na awamu zilizotangulia hasa rekodi nzuri ya uchumi mpana wa nchi, uwekezaji katika miundombinu na kufikia viwango vizuri vya ukuaji uchumi kwa wastani wa asilimia saba kwa mwaka.

“Nitaweka dhamira ya kuongeza viwango vya ukuaji hadi kufikia asilimia 12 kwa mwaka na kurekebisha uchumi ili kuwapa fursa Watanzania wote kushiriki katika maendeleo ya nchi yao.”

Alisema Serikali yake itafanya kazi katika maeneo manne, ikiwamo mabadiliko katika kilimo na shughuli za vijijini, kuanzisha viwanda kwa msukumo wa kuongeza thamani ya mazao ya kilimo na rasilimali.

Wasira alitaja kazi nyingine ambayo Serikali yake itafanya kama CCM itampitisha kuwa ni pamoja na kutengeneza fursa za ajira zenye hadhi kupitia biashara ndogondogo na za kati, kufanya uchumi wa huduma uwe wa kisasa ukiwamo utalii na sekta nyingine za huduma kama viwanda.

“Watu wengi wanategemea kilimo ili kuendesha maisha yao, kipaumbele cha juu kitakuwa katika mapinduzi ya kilimo na uchumi wa vijijini ili kufanya uwe na uzalishaji wa juu ambao utaleta mabadiliko katika maisha ya Watanzania,” alisema Wasira.

Ajira
Akizungumzia ajira kwa vijana, Wasira alisema anadhamiria mbali na kutazama ajira rasmi zenye mshahara, ataweka mkazo katika ajira na fursa za kupata kipato katika kilimo, biashara ndogondogo na huduma za uzalishaji viwandani.

“Kwa mujibu wa takwimu kutoka Wizara ya Kazi na Ajira, karibu vijana milioni moja wanaingia kwenye soko la ajira kila mwaka, lakini 200,000 tu ndiyo wanaoajiriwa. Huu uwiano mbaya kama hautashughulikiwa unaweza kusababisha matatizo ya kijamii na kisiasa,” alisema.

Uzalishaji viwandani
Wasira alisema ataweka kipaumbele cha juu katika kuleta mageuzi ya uchumi na kutengeneza ajira endelevu zenye hadhi na uanzishaji viwanda utapewa msukumo ili iwe injini ya chanzo cha ajira.

Uvuvi
Wasira alisema uwezekano wa kukua kwa sekta ya uvuvi inawezekana, kwani Taifa limejaliwa kuwa na pwani, maziwa na mito ambayo ataweka dhamira ya kuleta mabadiliko katika sekta hiyo ili iwe biashara yenye tija na kuongeza uzalishaji wa kipato kwa watu wengi wanaojishughulisha na uvuvi.

“Mkazo wangu utakuwa katika kuimarisha vitendea kazi na kukuza stadi za kiteknolojia ili uvuvi uwe na uzalishaji zaidi, kupanua masoko na kuhamasisha uongezaji wa thamani ili kukuza sekta ya uvuvi,” alisema Wasira.

Mapinduzi ya kilimo
Wasira alisema Watanzania wengi wanategemea kilimo ili kuendesha maisha yao, hivyo serikali yake itatoa kipaumbele cha juu katika mapinduzi ya kilimo na uchumi wa vijijini ili kufanya uwe na uzalishaji wa juu ambao utaleta mabadiliko katika maisha ya Watanzania.

“Kwa kuzingatia uwezekazo mkubwa ambao Tanzania inao katika kilimo na idadi kubwa ya watu wanaoishi vijiji asilimia 70 hadi 75 wanaendesha maisha yao kutokana na kilimo na uchumi wa vijijini, hivyo nitajitahidi kuendeleza sekta hii ili kuleta mabadiliko na kukifanya kilimo kiwe cha kisasa,” alisema.

Alisema anayo dhamira ya kuongeza ubora wa uzalishaji kwenye ngazi ya shamba ili kukuza kiwango cha vipato vya Watanzania walio wengi ambao wanajishughulisha na kilimo.

“Mikakati itakayotumiwa ili kuongeza uzalishaji kwenye kilimo ni kutumia njia bora za kilimo, sayansi na teknolojia na ubunifu kwa namna ya utafiti, huduma za ugani, miundombinu vijijini kama barabara, umeme na umwagiliaji. Katika mchakato huo uendelezaji masoko utapewa mkazo wa pekee ili kuhakikisha kinachozalishwa kinapata soko la uhakika,” alisema.

Picha na Aidan Mhando 
Chanzo : Mwananchi

Habari Zingine

0 MAOINI :

Fadhili Athumani



EastAfrica Swahili Blogger, Journalist at Mwanaspoti Kenya, Nairobi Kenya, Call: +254705246475, whatsapp:+255654724337, Email: fadhiliathumani85@gmail.com

Proudly Powered by EAMG .