TANZANIA: WAFANYABIASHARA WA SUKARI WAPAMBANA NA RAIS MAGUFULI
Posted in
afrika mashariki
,
Biashara
No comments
Sunday, February 28, 2016
By
danielmjema.blogspot.com
SASA ni wazi kwamba wafanyabiashara wa sukari nchini wameamua
kuanzisha vita na Rais John Magufuli, kwa kuamua kuficha bidhaa hiyo na
hivyo kuadimika katika soko na kupanda bei. Hatua hiyo ya wafanyabiashara imekuja baada ya Rais Magufuli
kutangaza utaratibu mpya hivi karibuni wa kutaka uagizwaji wa sukari
kutoka nje ufanywe na wazalishaji wa bidhaa hiyo hatua ambayo inakata
mrija wao wa ulaji.
Jana Bodi ya Sukari ililazimika kuitisha mkutano na waandishi wa
habari na kueleza kile walichokibaini baada ya kuwapo kwa taarifa kuwa
bidhaa hiyo imeadimika. Akitoa tamko kwa niaba ya Bodi ya Sukari na wazalishaji bidhaa hiyo,
Mwenyekiti wa bodi ya Wakurugenzi wa Kiwanda cha Sukari cha Kilombero,
Ami Mpungwe, alisema tangu Rais Magufuli alipotangaza utaratibu mpya wa
kuwatumia wazalishaji kuagiza sukari wamebaini kuwa baadhi ya
wafanyabiashara wameanza kufanya mipango ya kuhujumu taratibu hizo.
Alisema wafanyabiashara hao wameamua kuficha bidhaa hiyo ili
kuwaaminisha wananchi kwamba sababu kubwa ya kuadimika kwa sukari
inachangiwa na uamuzi huo wa rais. Kabla ya uamuzi huo haujafikiwa na Rais Magufuli, wafanyabiashara
wengi wa bidhaa hiyo walikuwa hawalipi kodi hali iliyochangia kufanya
biashara hiyo kiholela huku wakipata faida nyingi na kuinyima mapato
Serikali.
Hili linathibitishwa na kauli iliyotolewa na Mpungwe jana ambaye
aliwanyooshea vidole waziwazi wafanyabiashara hao kwamba walikuwa
wakinufaika na uingizaji holela wa sukari bila kulipia kodi na kwamba
hata wanachokifanya sasa cha kupandisha bei ya sukari ni mbinu chafu ili
kudhoofisha juhudi za Serikali za kuendeleza viwanda vya ndani kwa nia
ya kujinufaisha wao binafsi.
“Wameanzisha kampeni za kuwatia hofu wananchi wakiwaonyesha sukari
imeadimika kutokana na agizo lililotolewa na Serikali la kudhibiti
uingizaji sukari nchini,” alisema Mpungwe. “Miongoni mwa vitendo hivyo ni kuficha maghalani na kuendesha
propaganda kwamba bei ya sukari imepanda na wapo waliopandisha kwa
ghafla bei ya sukari kwa madai kwamba kuna upungufu viwandani na wengine
wakiwalaghai watu kwamba bei wanayonunulia viwandani imepanda,” alisema
Mpungwe na kusisitiza kuwa wanaofanya hujuma hiyo watachukuliwa hatua
za kisheria.
Akizungumzia utaratibu huu mpya alisema unafanyika kwa kuzingatia
ulipaji kodi kwa sukari ya nje inayoingizwa nchini lakini pia umelenga
kulinda viwanda vya sukari kwa kuimarisha soko la ndani.
Mwenyekiti huyo wa Bodi ya sukari nchini, alisema wazalishaji nchini
wanatambua kwamba viwanda vyote vya wasambazaji vinauza sukari kati ya
shilingi 1,700 na 1,800 kwa kilo na hakuna kilichopandisha bei tangu
tamko la Rais lilipotoka.
“Hali ya uzalishaji sukari msimu huu 2015/2016 ni nzuri na msimu
utafungwa Aprili kupisha matayarisho ya msimu mpya 2016/2017 Mei na Juni
2016 kama ilivyo taratibu kwa kila mwaka na viwanda vina akiba ya tani
32,000 za sukari inayoendelea kuuzwa,” alisema na kuongeza:
“Kiwanda cha sukari cha TPC kilichopo Moshi na kile cha Kagera
vinaendelea kuzalisha sukari hadi Aprili 2016 na Serikali imeshatangaza
utaratibu wa uagizaji wa sukari ambao utahakikisha sukari inayoruhusiwa
kuingizwa nchini na kiasi kinachohitajika kuziba mahitaji ya wakati
viwanda vinapokuwa vimefunga uzalishaji.”
Aliongeza kuwa kutokana na utaratibu huu mpya wa kuweka uwazi katika
usimamizi wa bidhaa ya sukari, utasaidia kwa kiwango kikubwa kudhibiti
sukari ya magendo na kuhakikisha inayoingia ni ile iliyoruhusiwa kwa
kulipiwa kodi.
Mwenyekiti huyo alisema Bodi ya sukari na wazalishaji
wanawahakikishia Watanzania kwamba hali ya upatikanaji wa sukari nchini
ni nzuri na wao kwa kushirikiana na vyombo husika vya Serikali
watahakikisha wanaendelea kuwa na sukari ya kutosha kwa muda wote.
KAULI YA RAIS MAGUFULI
Hivi karibuni Rais Magufuli alitoa kauli ya kupiga marufuku
uingizwaji wa sukari kutoka mataifa ya kigeni ili kuvilinda viwanda vya
sukari nchini ambavyo vimeathiriwa na uingizaji wa sukari ya bei rahisi
kutoka nje.Rais huyo alisema Taifa haliwezi kufikia malengo yake ya kuimarisha
viwanda vya ndani iwapo viwanda vya sukari nchini havitalindwa na
kuwezeshwa dhidi ya uingizaji huo.
Rais Magufuli alielezea kuwepo kwa viwanda nchini ambavyo hununua
miwa kutoka kwa wakulima wadogo wadogo na viwanda hivyo huzalisha
sukari, lakini pia ajira ni chanzo cha mapato ya Serikali. Alisema ingawa ipo hifadhi ya kutosha ya sukari lakini wapo watu serikalini wanaotoa vibali vya kuingiza sukari kutoka nje.
Aliwaelezea watu hao kama ni sehemu ya kukandamiza juhudi za Serikali
hali iliyosababisha kuchukua hatua ya kuzuia utolewaji wa vibali
kuruhusu uingizaji wa sukari, hadi itakapotokea mahitaji maalumu. Alisema wapo baadhi ya wafanyabiashara wasiowaaminifu ambao wamekuwa
wakiingiza sukari nchini iliyoisha muda wake wa matumizi na haifai
kutumiwa na binadamu.
Mahitaji ya sukari nchini ni tani 420,000 ambako tani 170,000
zinatumiwa kwa mahitaji ya nyumbani na nyingine iliyobaki hutumiwa
viwandani. Alisema viwanda vya hapa nchini vimekuwa vikizalisha tani 300,000
hali inayosababisha kuwepo kwa upungufu wa tani 290,000 kila mwaka kwa
matumizi ya nyumbani na yale ya viwandani.
Chanzo: Mtanzania
Mwandishi: Shabani Matutu
Habari Zingine
Mjulishe Mwenzako
0 MAOINI :