KONGAMANO LA USALAMA LAFANYIKA MJINI ADDIS ABABA, ETHIOPIA
Posted in
Uhalifu
No comments
Friday, April 15, 2016
By
danielmjema.blogspot.com
Kongamano kuhusu usalama lililopewa jina Tana, linafanyika Addis Ababa
Ethiopia. Litajadili masuala muhimu yanayoathiri mahusinao kati ya
Afrika na mataifa mengine ya dunia kuhusiana na ajenda ya usalama wa
dunia. Njia za kupambana na wanamgambo wa kundi la al Shabaab pia ni moja ya maswala yatakayojadiliwa.
Ni dhahiri leo, kuliko wakati mwingine wowote ule, kwamba Afrika inahitaji kuungana na kuzungumza kwa kauli moja kama inataka kuwa na ushawishi na kuyalinda masilahi yake katika mijadala ya kimataifa kuhusu usalama.
Kwa mara nyingine tena Kongamano la Tana litawapa fursa viongozi wa serikali na mataifa ya Afrika, maafisa wa vyeo vya juu wa serikali pamoja na watu mashuhuri, wasomi, viongozi wa sekta binafsi na wadau wengine, kulijadili kwa kina jukumu la bara la Afrika katika masuala ya usalama wa kimataifa.
Kauli mbiu hiyo ni muafaka, hususan wakati huu ambapo Afrika inaathiriwa na mitihani ya kiusalama. Bara hilo halikabiliwi tu na matatizo makubwa ya kiusalama, bali pia iko mstari wa mbele katika kutafuta njia za kukabiliana na matatizo ya kiusalama, yaliyosababisha hali ya wasiwasi ulimwenguni kote - kuanzia mizozo kuhusu raslimali hadi uhamiaji, mizozo ya ndani na changamoto za kusaidia operesheni za pamoja za kulinda amani.
Afrika yatakiwa kuwa na sauti moja
Masuala ya usalama hujadiliwa katika mikutano rasmi ya baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, mashauriano kati ya viongozi wa mataifa makubwa na makongamano maalumu ya kimataifa kuhusu kwa mfano mabadiliko ya hali ya hewa, mzozo wa kiuchumi, mazingira, mzozo wa chakula, nishati, usambazaji wa silaha za nyuklia na silaha za kibayolojia.
Katika baadhi ya mikutano hii Afrika huonekana kama eneo la kitisho kwa usalama wa kimataifa, umasikini, rushwa, ugonjwa wa ukimwi na virusi vinavyosababisah ugonjwa huo vya HIV, uhamiaji na matatizo mengine.
Sauti ya Afrika haijawahi kuwa sehemu ya mazungumzo ya aina hiyo kwa sababu kadhaa, zikiwemo za kisiasa, kiuchumi, kijeshi na kiteknolojia, ambazo zinavuruga uwezo ya bara hilo katika ngazi ya kimataifa. Ndio maana kuna haja ya Afrika kuandaa mkakati wa pamoja kuelekea ajenda za kigeni kuhusiana na usalama wake.
Kongamano la Tana 2016 mjini Addis Ababa linafanyika wakati bara la Afrika likiwa limejumuishwa katika mfumo wa usalama wa dunia. Mada muhimu kwa wadau wa Afrika na wa kimataifa ni ugaidi, itikadi kali za kisiasa na kidini, uharamia, ulanguzi wa dawa za kulevya na biashara haramu ya usafirishaji wa binaadamu na pia uthabiti wa mataifa ya Afrika, utawala bora na usimamizi mzuri wa masuala ya usalama.
Habari Zingine
Mjulishe Mwenzako
0 MAOINI :