Tuliwapa Salah na De Bryune 'Second Chance' iweje tusimpe Balloteli

No comments
Saturday, May 5, 2018 By danielmjema.blogspot.com

LONDON, ENGLAND


Ni ngumu kufananisha maji na mafuta, hilo halina ubishi, lakini kama Soka la Uingereza liliweza kumuamini Mohammed Salah na kumpa ‘second chance’, akaonesha alichonacho, kwanini ishindwe kumuamini mtukutu Mario Balotelli?

Kwanini ilikuwa rahisi kuamini kuwa Salah amebadilika halafu ishindwe kuamini kuwa Balloteli ameacha utukutu na kwamba sasa yuko tayari kucheza soka?

Mwaka 2011, Chelsea walitangaza kumsajili Mohammed Salah, kwa pauni milioni 11, lakini baada ya kushindwa kuonesha makali yake, akapelekwa Fiorentino na Roma kwa ahadi ya kurudi atakapo kuwa tayari kucheza
soka.

Ni kweli Salah, alipohakikisha ameiva, alirejea England, mwenyeji wake akiwa ni Liverpool. Salah akauhakikishia umma wa wapenda nchini England, kwamba sasa yuko tayari kucheza soka la uhakika. Tulimuamini na kilichotokea ni kama mlivyosikia.

Kama ilivyokuwa kwa Salah, Kevin De Bryune alitua England mwaka 2012, akitokea Ubelgiji. Akasajiliwa na Chelsea, lakini kwa bahati mbaya wakati huo, bado hakuwa tayari kucheza soka, ikabidi aondoke kwa ahadi
ile ile, ya kurejea atakapokuwa tayari.

Na kweli, mwaka 2015, baada ya kuzuruza kila mahali kutafuta uzoefu, De Bryune alirejea na kutua pale Etihad. Akatuaminisha kuwa ni kweli amebadilika na kama kawaida wapenda soka tulimuelewa tukampa ‘second
chance’. De Bryune hajatuangusha kuanzia hapo.

Unaweza kujiuliza ni  kwanini nimewataja wanaume hawa, wakati muhusika ni Super Mario Balloteli. Ni hivi, kati ya mwaka 2010 na 2013, Balloteli alikuwa mchezaji wa Manchester City, hata hivyo hakukaa, akaondoka.

Kilichomuondoa Balloteli pale Etihad (City of Manchester), hakina tofauti sana na kilichowaondoa De Bryune na Salah wakati ule; hakuwa tayari kucheza, tena yeye kesi yake ilikuwa tofauti kwa maana kwamba, alikuwa amezidiwa na ‘utoto’

Mwaka 2013, baada ya kuondoka England alielekea Italia ambako alijiunga na AC Milan. Akaichezea jumla ya michezo 43 na kufunga mabao 26. Mwaka 2014, akiamini yuko vizuri, alirejea England na kutua Liverpool. Hata hivyo, hakuwa na jipya, katika mechi 16, aliishia kufunga bao moja tu.

Liverpool, wakamuambia akajifue akiwa tayari watamfikiria. Wakamrudisha AC Milan kwa mkopo. Aliporejea AC Milan, Balloteli aliwaomba radhi wapenzi wa mchezo wa soka duniani kote na kuwahakikishia kuwa amebadilika na yuko tayari kucheza soka.

Akizungumzia mchezaji huyo, Kocha wa Liverpool wakati huo, Brendan Rogers, alituhakikishai namna ambavyo Balloteli amebadilika na yuko tayari kucheza soka. Alisema Muitaliano huyo sasa amekuwa na kwamba ameacha utoto. Wote walitundanganya!

Akaingia dimbani mara 20 na kufunga bao moja. Mwaka 2016, Liverpool ikampiga bei mazima katika klabu ya Nice, inayoshiriki Ligue 1, nchini Ufaransa. Kuanzia hapo akaanza kuonesha kubadilika, katika mechi 46, amefanikiwa kufunga mabao 29!

Akiwa na miaka 27, Balloteli sasa hivi anaonesha dalili za kupevuka. Baada ya kukaa nje ya soka la ushindani kwa zaidi ya miaka miwili, haimanishi kwamba Ligue 1 hakuna ushindani, lakini kwa kuzingatia mwenendo wa soka la Balloteli, ashakum sio matusi, alikuwa lupango.
 

Muitaliano huyu, hivi sasa anaonesha utayari wa kurejea kwenye ulimwengu wa soka. Msimu huu ameingia dimbani mara 33 na kufumania nyavu mara 22. Huu ni muendelezo wa alichokifanya msimu uliopita ambapo alifunga mabao 15, katika mechi 23.

Yote hayo Balloteli ameyafanya bila ya kujikuta katika matukio ya kitoto kama kupigana klabuni. Ili kuthibitisha kuwa kwa kweli amebadilika, hakuna siku hata moja amejikuta akiingia katika mvutano na kocha wake wala wachezaji wenzake.

Kuna tetesi kuwa, Muitaliano huyo yuko tayari kurejea England. Hapa ndipo hoja yangu inapoanzia, Endapo itathibitika kuwa ni kweli Balloteli anataka kurudi England, Je tutakuwa tayari kumpokea na kumpa ‘second chance’ kama tulivyofanya kwa Salah na De Bryune?

Kuna madai kuwa, Jose Mourinho anafikiria kumrejesha nyota huyo wa zamani wa Manchester City na Liverpool. Kama hilo litatokea itakuwa ni habari nzuri. Lakini swali ni je tunaweza kumuamini Balloteli? Akirudi
ataendeleza moto wake, au atafufua vituko vyake?

Hivi sasa anachokifikiria ni kushiriki michuano mikubwa. Balloteli anawaangalia Mohammed Salah na Kevin De Bryune na kujikuta akitamani kupata mafanikio makubwa katika soka, ikizingatiwa kuwa, umri wake
haumpi uhakika wa kuendelea kuwa na kiwango alichonacho sasa baada ya miaka miwili.

Ukweli huu ndio unaowapa hofu viongozi wa Nice na benchi la ufundi la klabu hii kwa sasa. Wanafahamu kuwa hawana uwezo tena wa kumpa anachokitaka katika umri huu wa miaka 27. Kwa sasa Balloteli anahitaji
mafanikio, anataka kubeba mataji. Rais wa Nice, Jean-Pierre Rivere, analithibitisha hilo:

“Bila mashinano ya Ulaya, itakuwa ngumu kumshawishi kwa sasa, ni wazi kuwa hatuna nafasi ya kucheza ligi ya mabingwa, Kombe la Uropa nao ni mfupa mgumu kwetu, kwa hali naona akiondoka, ni moto wa kuotea mbali
uwanjani, amebadilika sana, hata staili yake ya uchezaji umebadilika pakubwa.”

Kama kuna kitu cha kujifunza kutoka katika msimu huu wa soka wa ligi kuu ya England, ni kwamba hata nyota wenye majina makubwa, huwa wanahitaji muda na changamoto ya kuwajenga na kuwafanya wawe na ubora
walioa nao.

Mfano hai ni Kevin De Bryune wa Man City na Mohammed Salah wa Liverpool. Hata Cristiano Ronaldo mwenyewe ilibidi aondoke Sporting Lisbon, apitie katika mikono salama ya Sir Alex Ferguson kabla ya kuwa staa wa dunia tunayemshudia pale Santiago Bernabeu.

Kama kigezo cha umri ndicho kitakachosababisha soka la England na mashabiki wake wamkatae Balloteli kwa sasa, basi kuna haja ya kurudi maktaba na kutafuta kitabu cha Jamie Verdy, kulisoma na kuelewa maana
halisi ya mafanikio na Umri.

Kama Verdy aliweza kuipa Ubingwa Leicester katika umri wake mkubwa wa miaka 30, kwanini ishindikane kwa Balloteli na miaka yake 27? Maana yangu ni kwamba hakuna umri maalum, au wakati maalum wa kufanya
kilichosahihi.

Mario Balloteli Barwuah, wa sasa sio yule tuliyemzoea, Balloteli wa sasa ni Baba wa watoto wawili, Lion na Pia. Anarudi kwetu akiwa ni mtu mzima. Anajua ni kipi kinachomstahili kama Baba wa familia. Huu ndio wakati ambao tunaweza kukishuhudia kipaji halisi cha Balloteli. Majukumu aliyonayo yanamsukuma kujituma.

Mwenyewe amekiri kuachana na zile tabia za kupgana Baa. Amekiri kuachana na tabia za kukimbizana na vibinti vidogo katikati mwa Jiji la London na Manchester kama ambavyo alizoea kufanya kipindi. Anasema kabadilika kwanini tushindwe kumuamini kama tuliweza kuwaamini Salah na De Bryune?

Mwisho.

Habari Zingine

0 MAOINI :

Fadhili Athumani



EastAfrica Swahili Blogger, Journalist at Mwanaspoti Kenya, Nairobi Kenya, Call: +254705246475, whatsapp:+255654724337, Email: fadhiliathumani85@gmail.com

Proudly Powered by EAMG .