WAONGOZA WATALII MLIMA KILIMANJARO WALIA NA SERIKALI MALIPO MADOGO
Posted in
Utalii
No comments
Monday, May 19, 2014
By
danielmjema.blogspot.com
Meneja wa TTB tawi la Arusha, Willy Lyimo akimpa mkono mmoja wa wahitimu wa mafunzo ya huduma ya kwanza. |
Mgeni Rasmi, Katibu Tawala wa wilaya ya Arumeru, Evaliliana francis akiwatunuku wajhitimu wa mafunzo ya huduma ya kwanza iliyotolewa na Red Cross kwa kushirikiana na KGA |
Mhazini wa KGA, Gerald Francis baada ya kukabidhiwa cheti chake |
Katika picha ya Pamoja |
Na Mwandishi wetui, Arusha
CHAMA cha waongoza watalii mlima Kilimanjaro (KGA), kimeitaka serikali na mamlaka husika kuweka bayana viwango vya malipo wanayostahili kulipwa waongoza watalii badala ya sasa, ambapo kila kampuni inalipa
inavyojua.
Rai hiyo imekuja wakati ambapo taarifa zinaeleza kwamba pamoja na serikali kupitia wizara ya maliasili na utalii mwaka jana kupitisha kima cha chini kinachotakiwa kulipwa kwa waongoza watalii kuwa dola 20, kuna makampuni ambazo zinadaiwa kulipa Dola 10 hadi 5 kwa siku.
Akizungumza katika hafla ya kutunuku vyeti kwa waongoza watalii 84 waliohitimu mafunzo ya huduma ya kwanza, Mwenyekiti wa chama hicho, Respicious Bhaitwa alisema serikali inatakiwa kuingilia kati urasimu
huo ambao unatishia maendeleo ya sekta ya utalii nchini.
Bhaitwa alisema kuna haja ya serikali kupanga kiwango ambacho
kitatumika na makampuni yote kulipia waongoza watalii na kubainisha kuwa hiyo itasaidia kuboresha sekta hiyo na kuifanya bora katika uchangiaji wa pato la taifa.
"Baadhi ya makampuni yameanzisha vikundi vidogo ambavyo vinatumika kudhoofisha umoja wa waongoza watalii, malipo ni ya chini, lakini pia hata hicho kidogo hakitoki kwa wakati sahihi, tunaiomba serikali
kuingilia kati na kupanga kiwango sahihi," alisema Bhaitwa
Alisema katika kuhakikisha hilo ipo haja ya wizara ya maliasili na utalii kushirikiana na KGA katika kuwaendeleza waongoza watalii kwenye mlima wa Kilimanjaro na Meru, ili waweze kuwatumikia katika mkakati wa kuongeza idadi ya watalii na kuboresha utalii wa Tanzania hususani hifadhi za milima.
Kwa upande wake meneja wa Bodi ya Utalii (TTB) tawi la Arusha, Willy Lyimo aliwataka waongoza watalii kujiendeleza kitaaluma kama njia ya pekee ya kutatua matatizo yanayojitokeza kwa sasa.
Alisema ili kupata mafanikio makubwa katika shughuli zao pamoja na kupata heshima stahiki katika jamii ni lazima wazingatie suala la Elimu kwani hata malalamiko ya Malipo yanatokana na Makampuni kuwadharau kwa sababu ya elimu zao duni.
Naye mwakilishi wa Mkuu wa wilaya ya Arumeru, ambaye ndiye alikuwa Mgeni rasmi katika hafla hiyo, Katibu Tawala wa wilaya hiyo, Evaliliana Francis alisema Serikali bado inazingatia wazo lake la kuboresha sera ya utalii ya mwaka 1999 ili kuifanya kuendana na mahitaji ya sasa.
Aidha katika kuhakikisha kinapunguza matukio ya kiusalama kwa watalii zaidi ya 2500 wanaopanda mlima kilimanjaro kila siku, chama cha Msalaba mwekundu (Red Cross) kwa kushirikiana na chama cha waongoza
watalii mlima Kilimanjaro (KGA), kimeanzisha utaratibu wa kutoa mafunzo ya huduma ya kwanza kwa waongoza watalii mlimani hapo.
Utaratibu huo ambao umeanza mwaka huu unalenga kupunguza matukio kama vile kukwama kwa watalii mlimani hapo, ambayo yamekuwa yakitishia maendeleoa ya sekta hiyo inayoshika namba mbili kwa uchangiaji wa pato la taifa kwa sasa.
Akizungumza kuhusu utaratibu huo, Bhaitwa alisema wamefikia hatua hiyo kutokana na kutambua kuwa waongoza watalii ndio mabalozi wa taifa kwa wageni hao wanaopanda mlima huo kila siku
Bhaitwa alisema katika utaratibu huo pia chama hicho kimepanga kutoa elimu ya Lugha mbalimbali za kimataifa kwa waongoza watalii kama njia ya kuwawezesha kutoa huduma bora kwa watalii na kukuza utalii hapa
nchini na hasa katika hifadhi ya milima.
"Waongoza watalii wanafanya kazi kubwa, nzuri na ngumu ya kuongoza maelfu ya watalii katika mlima Kilimanjaro na Meru na kuifanya hifadhi ya mlima Kilimanjaro kuwa hifadhi ya kwanza kati ya hifadhi takribani 16 kwa kuingiza pesa nyingi za kigeni," alisema Bhaitwa
Jumla ya waongoza watalii 84 kutoka Moshi (31), Arusha (35) na Marangu (18) walitunukiwa vyeti hivyo ambapo malengo kwa mujibu wa risala ya chama hicho yalikuwa ni kutoa mafunzo kwa wanachama 300 kati ya 1060
katka awamu ya kwanza.
Mwisho.
Habari Zingine
Mjulishe Mwenzako
0 MAOINI :